Mwandishi Wetu
Profesa Ibrahimu Lipumba |
KILIO cha hali ngumu ya maisha tangu
kuanza kwa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, kimemgusa mwenyekiti wa Chama
cha Wananchi (CUF), anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa
nchini, Profesa Ibrahim Lipumba.
Profesa Lipumba ametoa wito maalumu kwa
Rais John Magufuli kusikiliza kilio hicho cha wananchi kwa kulegeza kamba ya
kubana matumizi na kuwaandalia wananchi mazingira mazuri ya kumudu maisha yao.
Profesa Lipumba alitoa wito huo juzi katika
mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea Udiwani wa Kata ya Kijichi iliyoko Temeke
jijini Dar es Salaam kupitia chama hicho, Khalid Shamas.
Lipumba ambaye ni profesa aliyebobea
katika taaluma ya uchumi, alisema sera ya kubana matumizi haina ubaya, lakini
jambo hilo, lazima liendane na mpango wa kuwasaidia wananchi katika kujipatia
riziki zao.
“Watu wanapigika na wengine wanalazimika
kufunga bila kunuia, halafu tunajigamba tumefanikiwa kukusanya fedha nyingi kwa
kubana matumizi. Hiyo inatusaidia nini wapiga kura wako, mheshimiwa rais?”
alihoji Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba ambaye aliwahi kuwa
mshauri wa mambo ya uchumi katika Serikali ya Awamu ya Pili na mtaalamu
aliyewahi kutumiwa na mataifa mengi, ikiwamo Uganda kushauri masuala ya uchumi,
alisema uchumi unaokua bila kuonekana mifukoni mwa watu hauna tija.
“Hizo sera (za kubana matumizi) zinaweza
kuwa nzuri sana, lakini umesahaulika mpango wa kuona ni kwa namna gani wananchi
wanasaidiwa kumudu maisha yao. Leo vijana wanapigika na hakuna msaada.”
Profesa Lipumba aliishauri Serikali
kuwatengenezea wananchi mazingira mazuri ili waweze kuboresha maisha yao na
kujenga mazingira ya kutafsiri ukuaji huo wa uchumi katika maisha ya wananachi
wa kawaida.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Profesa
Lipumba imekuja ikiwa tayari Rais Magufuli ameeleza kuwa mpango huo wa kukata
mirija ya upatikanaji fedha kiholela, umelenga kuwafanya watu wafanye kazi.
Rais Magufuli ambaye Serikali yake
inaongozwa kwa kauli mbiu ya ‘hapa kazi tu’ alisema anataka kila Mtanzania ale
kwa kipato chake halali. Akaamua kusitisha vikao na semina za taasisi za
Serikali mahotelini na kupunguza safari za nje za mawaziri, huku akiboresha
ukusanyaji kodi kama moja ya hatua ya kutaka taifa lijitegemee.
Amnadi
mgombea wake
Profesa Lipumba aliwaomba wakazi wa
Kijichi kumchagua Khalid Shamas kuwa diwani wa kata hiyo katika uchaguzi mdogo
uliopangwa kufanyika Januari 22, ili apeleke kilio cha ugumu wa maisha katika
vikao vya halmashauri.
“Siyo rahisi CCM kusema ukweli kuhusu
jambo hilo. Hapa tunahitaji mtu mwenye misimamo tofauti kidogo. Mchagueni
Shamas akawakumbushe CCM kwamba pamoja na mipango yake, watu wanapigika… Hakiii...”
Akizungumza katika mkutano huo, Shamas
aliomba achaguliwe akieleza kuwa amekuja na mipango mbadala ya kuwaletea wakazi
wa Kijichi maendeleo endelevu.
“Wagombea wote hakuna aliyefika hapa na
kablasha la kazi. Mimi ninalo, hili hapa,” alisema Shamas akionyesha karatasi
aliyoishika mkononi.
Aliendelea “Humo kuna mambo mengi.
Mkinichagua nitaanza na elimu. Nitahakikisha nasimamia sera ya CCM ya elimu
bure itoe elimu bora na siyo bora elimu. Nitasimamia ujenzi wa maabara katika
shule zote za Sekondari, ujenga soko katika kila mtaa, mabweni kwa wanafunzi wa
kike na umeme mashuleni.
Uchaguzi mdogo wa Kijichi unafanyika
kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo kupitia CCM, marehemu Underson
Charles.
0 comments:
Post a Comment