NYUMBA 711 kati ya 1, 000 za makazi
zimejengwa kwa ajili ya watumishi wa umma hadi mwishoni mwa mwaka jana.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Watumishi Housing
Company (WHC), Dk Fred Msemwa alibainisha hayo jana alipozungumza na mwandishi
wa habari hizi.
Dk Msemwa alikuwa akitoa tathmini ya
miradi ya ujenzi wa makazi kwa watendaji wa Serikali chini ya kampuni hiyo inayosimamia
miradi 20 kwenye mikoa kadhaa nchini ambapo Sh bilioni 36 zinatarajiwa kutumika
hadi kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo.
Alisema nyumba hizo 711 ziko tayari
kuuzwa kwa kila mtumishi wa umma kuanzia mwezi huu.
Dk Msemwa alisema nyumba zinazojengwa
chini ya miradi hiyo zinauzwa kati ya Sh milioni 33 na Sh milioni 76.
Alitaja baadhi ya miradi ambayo iko
tayari kuwa ni ya Dar es Salaam maeneo ya Bunju, Gezaulole na mkoani Morogoro.
“Tayari tumeanza ujenzi wa nyumba za bei
nafuu ambazo gharama zao hazizidi Sh milioni 25. Tumeanza kujenga nyumba 90
katika mikoa saba kwa ushirikiano na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),” alisema
Dk Msemwa.
Alitaja baadhi ya changamoto zinazoonekana
kuwa kikwazo kwa watarajiwa wa makazi hayo, kuwa ni riba kubwa inayotozwa na
taasisi za fedha.
Alifafanua kuwa riba hiyo inafanya
watumishi wengi wa umma kushindwa kuhimili makato ya kila mwezi kwenye
mishahara yao.
Alisema malengo ya kampuni hiyo ambayo
iko chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ni kufikia
wananchi wa kada zote za maisha.
Alisema miaka mitatu ijayo baada ya
kupata tathmini kamili kupitia miradi wanayoendelea nayo sasa, watajikita
katika ubunifu wa nyumba za bei nafuu
zaidi ili kufikia Watanzania wote wakiwamo wa kipato cha chini.
0 comments:
Post a Comment