Hussein Ndubikile
Dk Anna Senkoro |
MWILI wa aliyekuwa mgombea urais wa
kwanza mwanamke nchini katika Uchaguzi Mkuu wa 2005 kupitia chama cha TPP-Maendeleo,
Dk Anna Senkoro, unatarajiwa kuzikwa kesho kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es
Salaam.
Dk Senkoro alifariki dunia ghafla juzi,
wakati akipelekwa kupewa matibabu ya ugonjwa wa moyo kwenye Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili (MNH).
Akizungumza na gazeti hili jana, mdogo
wa marehemu, George Sendimu alisema mwanasiasa huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi
kwa muda mrefu na wiki mbili zilizopita alikuwa akihudhuria kliniki kwenye
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam.
“Tumepokea msiba kwa masikitiko makubwa
ila tunamshukuru Mungu kwa yote, matatizo ya moyo yalimsumbua muda mrefu hata
juzi (Jumanne) alikwenda kliniki Muhimbili,” alisema.
Alisema siku mbili zitakuwa za
maombolezo nyumbani kwa marahemu Tabata Segerea-Mzimuni huku akiongeza kuwa Jumamosi
mwili utaagwa na kufanyiwa maombi saa 6 mchana kwenye Kanisa la Winners Chapel
International lililoko Banana, Ukonga karibu na shule ya msingi ya Minazi
Mirefu na kuzikwa saa 8 mchana.
Mtoto wa pili wa marehemu, Joan Japhet
alisema ameguswa na kifo hicho kwa kuwa mama yake alikuwa mtu wake wa karibu na
watu wengine, kwani aliwaonesha upendo wa dhati.
Mchungaji wa Kanisa hilo, Samwel Adeyemi
alisema marehemu alipenda kumtumikia Mungu na alikuwa mwenye upendo kwa watu na
kuiomba familia kuendelea kudumisha mshikamano katika kipindi hiki kigumu.
Mbunge wa zamani wa Segerea na Naibu
Waziri wa Wizara ya Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga alisema marehemu
alikuwa kiongozi mwanamke shupavu na mpenda maendeleo na hata katika uchaguzi
wa mwaka juzi alifanya kazi kubwa ya kuzunguka mikoani kuwahamisha wanawake.
Alisema alikuwa na marehemu CCM na wakahamia
wote Chadema na mpaka mauti yanamkuta alikuwa Mwenyekiti wa Emmas Saccos ya
Segerea inayotoa mikopo kwa wanawake kuwakomboa kutoka kwenye wimbi la umasikini.
Aliomba viongozi kujenga utamaduni wa
kupima afya mara kwa mara ili kujua hali zao huku akiwashauri kukubali ushauri
wa madaktari, kwani huenda mauti yasingemkuta kutokana na kukataa ushauri wa kulazwa
hospitalini hapo Jumanne.
0 comments:
Post a Comment