Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, leo
inatarajia kutoa hukumu dhidi ya
waliokuwa vigogo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA).
Vigogo hao ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim
Mgawe na Naibu wake, Hamadi Koshuma, ambao walishitakiwa kwa matumizi mabaya ya
madaraka.
Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Cyprian Mkeha wa Mahakama hiyo, baada ya kusikiliza ushahidi wa
mashahidi wa upande wa Jamhuri, utetezi, vielelezo, majumuisho ya mwisho na
sheria inayohusu mashitaka hayo.
Ilidaiwa kuwa Desemba 5, 2011, washitakiwa watumishi TPA
ambapo katika utendaji wao kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kwa
kusaini mkataba wa kibiashara bila kuitisha zabuni.
Mkataba huo ulikuwa baina ya TPA na kampuni Communication
and Construction ya China (CCCC), ambao ukihusu ujenzi wa gati namba 13 na 14.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa kitendo hicho ni kinyume na
kifungu cha 31 cha Sheria ya Ununuzi namba 21 ya 2004 na ikidaiwa kililenga
kuinufaisha CCCC. Baada ya kusomewa mashitaka,
walikana kuhusika na tuhuma hizo.
Vigogo hao wako nje kwa dhamana ya wadhamini wawili
waliosaini bondi ya Sh milioni mbili kila mmoja kiasi hicho hicho.
Katika utetezi wake Mgawe alikana kukiuka sheria za
ununuzi wa umma akidai alisaini mkataba kwa makubaliano ya masharti ya mkopo
kutoka benki ya Exim ya China, pia alisaini
makubaliano ya kibishara na kampuni hiyo na si mkataba wa ujenzi wa gati namba
13 na 14 katika bandari ya Dar es Salaam kama inavyodaiwa.
Akiongozwa na Wakili Frank Mwalongo, Mgawe alidai kuwa TPA
ilitangaza zabuni ya kupata upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa gati hizo na
ilipatikana kampuni ya CPCS ya Canada.
Alidai kuwa baada ya upembuzi yakinifu ilibainika kuwa
ujenzi huo utagharimu dola milioni 321 za Marekani na kupendekeza ujenzi huo
uwe wa ubia na hivyo kuingia mkataba na CCCC ambayo iliahidi kufanikisha
upatikanaji wa mkopo.
0 comments:
Post a Comment