Waandishi Wetu
MMOJA wa wakurugenzi watatu wa Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco) walioshushwa vyeo juzi, Decklan Mhaiki ambaye
alikuwa Naibu Mkurugenzi wa Uwekezaji, amesema yuko tayari kufanya kazi kokote ndani
ya shirika hilo.
Mhaiki na wenzake; aliyekuwa Mkurugenzi
wa Usambazaji, Sophia Mgonja na Johary Kachwamba aliyekuwa Mkurugenzi wa
Uzalishaji walishushwa vyeo siku tano tu baada ya Rais John Magufuli kutengua
uteuzi wa Felschemi Mramba aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo.
Juzi taarifa za kuondolewa kwenye nafasi
hizo zilivuja kutoka ndani ya shirika hilo ikiwa ni baada ya Mwenyekiti wa Bodi
ya Tanesco, Dk Alex Kyaruzi kukutana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
hilo, Dk Tito Mwinuka.
Jana Msemaji wa Shirika hilo, Leyla
Muhaji alipoulizwa sababu za kuondolewa kwa wakurugenzi hao alisema itatolewa
taarifa rasmi kwenye vyombo vya habari, ambayo pamoja na mambo mengine
itafafanua kwa kina suala hilo. Hata hivyo alishindwa kuweka wazi taarifa hiyo
itatolewa lini.
Awali gazeti hili liliwasiliana na Dk Kyaruzi
na kuthibitisha kuwa sababu zipo licha ya kutokuwa tayari kuzitaja kwa maelezo
kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Bodi, si msemaji wa shirika
hilo.
Wakati Mhaiki akieleza hayo, wachambuzi
waliozungumza na gazeti hili waliishauri Serikali kuunda tume kuchunguza sababu
za Tanesco kushindwa kujiendesha kisasa na kusisitiza kuwa tatizo la shirika
hilo si watendaji bali mfumo waliodai kuwa unapaswa kubadilishwa.
“Sina cha kusema. mimi ni mwajiriwa
ninapangiwa kazi na mwajiri wangu. Hata kama ungekuwa wewe ungesema jambo gani?”
Alihoji Mhaiki.
Alipoelezwa lengo la kuulizwa jambo hilo
alisisitiza: “Ukiwa mwajiriwa kazi unapangiwa. Mwajiri akikupangia kitu kingine,
wewe unakuwa huna cha kusema zaidi ya kufanya.”
Sintofahamu ndani ya shirika hilo
iliibuka baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura)
kukubali maoni ya Tanesco ya kupanda kwa bei ya umeme kuanzia Januari mosi kwa
asilimia 8.5.
Hatua hiyo ilizuiwa na Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, huku Rais Magufuli akisema hatua hiyo
ilikuwa inakwamisha mipango ya Serikali inayojiandaa kuelekea kwenye uchumi wa
viwanda.
Desemba 31 Profesa Muhongo alizuia kupanda kwa bei hiyo, siku
moja baadaye Rais Magufuli amatengua uteuzi wa Mramba huku juzi wakurugenzi hao
wakishushwa vyeo.
Wachambuzi
Profesa Abdallah Safari ambaye kitaaluma
ni mwanasheria, alisema kitendo cha wakurugenzi hao kushushwa vyeo sambamba na Mramba
kutumbuliwa, kulitokana na Tanesco kuomba ridhaa ya kupandisha bei ya umeme,
jambo ambalo lilifanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Kuna mchezo unafanyika bila wananchi
kujua, ongezeko lililoombwa na Tanesco lingeweza kuinufaisha Serikali kwenye
kodi na wao walijua…mbona yapo mashirika na taasisi zingine za Serikali
zinapandisha bei katika mambo wanayoyasimamia na hawaguswi?” Alihoji.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM) Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema: “Yapo mambo mengi yaliyojificha
ndani ya Tanesco. Kama isipoundwa tume huru ya kuchunguza yanayoendelea na kuja
na hatua, hali itaendelea kuwa ile ile tu. Shirika haliendeshwi kisasa na
taaluma haizingatiwi zaidi ya siasa tu.”
Aliishauri Serikali kuboresha uzalishaji
wa gesi kwa maelezo kuwa ndiyo mbadala wa kuondokana na umeme wa maji.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Profesa Mwesiga
Baregu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (Saut) na kusisitiza: “Kama
ilivyoundwa tume kuchunguza sakata la kutoweka kwa faru John, pia Tanesco
inapaswa kuundiwa tume ili kujua kiini cha tatizo, kwa nini kila mwaka ina
matatizo yaleyale?”
Alisema shirika hilo linakabiliwa na
tatizo la kimfumo ambao ni lazima ubadilishwe.
0 comments:
Post a Comment