Salha Mohamed
Dk Valentino Mokiwa |
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi
ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa, amesema mgogoro katika Dayosisi hiyo ni
wa kutengenezwa na hauna uhalisia.
Mokiwa alisema hayo jana, siku moja
baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Jacob Chimeledya kudai kumng’oa
madarakani.
“Mambo mengi ya kutengenezwa, yametengenezwa
huko baa Sinza na kusainiwa barabarani humo. Mimi mwenyewe Desemba 18 mwaka juzi
niliwaita watu hawa nikae nao lakini walikimbia,” alisema Mokiwa.
Hata hivyo, alipotafutwa jana
kuzungumzia kauli ya Mokiwa, Askofu Mkuu Chimeledya ambaye alinukuliwa akisema
iwapo Askofu huyo atasema lolote, yeye (Askofu Mkuu), ‘atamwaga mboga’ alisema:
“Sipo tayari kuendeleza malumbano wala
mgogoro. Mimi nilishatoa taarifa yangu imetosha, pale kwamba anaipokea au
haipokei, andikeni alichosema lakini sitaki kutoa mawazo katika aliyosema.”
Alisema taarifa yake ilishasema na hawezi
kurudia, hivyo muhimu si mabishano bali maisha ya waumini na haitakuwa hekima
viongozi kugombana huku vyombo vya habari vikiandika.
“Andikeni alichosema yeye, mimi sitaki
kusema chochote, lakini kwa afya ya Kanisa sitaki kulumbana kwenye vyombo vya
habari,” alisema.
Aliwataka waumini watulie na wapo
watakaopima mambo na kuona au kuelewa nini kinaendelea, huku akibainisha kuwa
Kanisa halitakufa.
“Kanisa litaendelea, halifi leo….halifi,
ila tunaweza tukachochea watu wakapigana kwa kutumia njia zisizo sahihi na mimi
nilishasoma barua na ujumbe ulifika inatosha,” alisema.
Hata hivyo, Mokiwa alieleza kumshangaa
Askofu Mkuu kufika wakati wa kikao cha Halmashauri ya Kudumu akiwa na askari
wenye sare takribani 12 huku ikiwa ni mara ya kwanza kukutana na Halmashauri ya
Dayosisi hiyo.
“Alitushangaza akiwa na ujio wa askari
12 waliovaa sare, kilichomleta ni jambo aliloliita kuwa mrejesho, lakini
aliishia kusoma barua ya kudai ameniondoa kwenye madaraka ya huduma ya uaskofu.
Alisema baada ya Askofu Mkuu kutoa kauli
hiyo, Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi hiyo ambayo Askofu Mkuu hakuwahi kukutana
nayo, haikukubaliana naye.
Mokiwa alisema Halmashauri ya Kudumu
haikuwahi kupeleka mgogoro au machafuko ya Dayosisi hiyo kwani Askofu ndiye
anafanya kazi na Halmashauri hiyo.
Alisema Askofu Mkuu Chimeledya amekuwa
na makundi anayofanya nayo kazi bila kufuata utaratibu wa Kanisa.
“Kwa nini Askofu Mkuu kufanya kazi na
watu ambao si sehemu ya mamlaka halali ya Dayosisi ya Dar es Salaam?
Halmashauri ya Kudumu ilimwambia kuwa aliyozungumza kwenye kikao hicho ni
batili na wana Askofu mmoja ambaye ni Mokiwa,” alisema.
Alisema alichozungumza kwenye kikao cha
Halmashauri ya Kudumu kina upungufu kwani hapaswi kuwa nje ya Nyumba ya Maaskofu na kufanya kazi nje ya taratibu zao.
Askofu Mkuu ana timu yake ya maofisa,
lakini katika hili walimshauri vibaya, vyote vimekosewa katika kusimamia
taratibu zake.
Mokiwa alisema Askofu Mkuu, hakuingia
kwa mujibu wa taratibu na usimamizi na uendeshaji wa Kanisa hilo “Dayosisi ya
Dar es Salaam haina mgogoro na mimi ndiye Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es
Salaam, mgogoro wanaosema ni wa kutengenezwa,” alisisitiza.
Alisema kutokana na hayo yote anaweka
msimamo wa kuwa yeye ndiye Askofu wa Jimbo hilo, ingawa yaliyofanywa ni magumu
kwake, huku yakisemwa vibaya.
“Wale ni binadamu na kazi yangu mimi ni
kuwaombea nami nimewasamehe na sina tatizo na yeyote katika wao, huo ndio
msimamo wangu,” alisema.
Aliomba msamaha kwa jamii ya Anglikana
na wana imani nchini kwamba taasisi za dini hazipaswi kufanya mambo ya aina
hiyo kwani ni aibu.
Mokiwa alisema bado wanahitaji kujenga
umoja na kuondokana na migogoro ya kutengeneza na vita ya kuwaaibisha hivyo
makanisa na waumini watulie.
“Niwahakikishie wananchi kuwa hakutakuwa
na mgogoro wowote mimi ni Askofu wa Dar es Salaam sijaomba msaada wa polisi
katika mizunguko yangu, sijalindwa wala kula chakula mahali kokote, nina imani
na wananchi wa Dayosisi, kwamba tukisimama pamoja tutayashinda,” alisema
Mokiwa.
Mbali na maelezo hayo, Mokiwa alitaja
aliodai walitengeneza mgogoro na kusababisha yeye kufukuzwa kuwa ni Mshauri wa
Askofu Mkuu, Makamu wa Askofu Mkuu, Dayosisi ya Newala, Katibu Mkuu wa Kanisa
la Anglikana Tanzania ambaye pia ni Padri kwenye Dayosisi ya Morogoro.
“Hapa Dar es Salaam Askofu wetu mkuu
anafanya kazi na Kanisa la Andrea Mtakatifu Magomeni, ambako kuna mtu tulimwondolea
haki ya kisakramenti, baada ya kukiuka utii kwa kugoma kuhama,” alisema.
Mokiwa alimtaja mwingine kuwa ni
aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Uinjilisti, Utume katika Dayosisi hiyo ambaye pia
alimtoa kutokana na mambo ya kifedha na uaminifu kwa kujikopesha kutoka Saccos
ya Kanisa.
Mokiwa alisema mtu huyo aliondolewa kwa
alichodai kuwa ni utapeli baada ya kukopa na kukimbia kulipa madeni katika Benki
ya Afrika (BOA), Benki ya Akiba na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) kwa kutoa
picha zake.
“Sikutaka kuzungumza wakati wowote,
lakini sasa imebidi niseme kwa hao wanaotumika na Jimbo.
“Kanisa letu lilishawahi hata kuandikiwa
na Serikali kuwa linaongoza kwa migogoro ambayo mingi ni ya kutengeneza, ili
kusiwepo maelewano baina ya waumini na Askofu ili kusitawalike na wakubwa waingie
kushika hatamu hapa, hilo tunalijua,” alisema Mokiwa.
Alisema uongozi wa Kanisa umeingia
kufanya kazi kando ya utaratibu na kuleta maumivu kwa kumgonganisha Askofu na
watu anaowaongoza.
Alisema uongozi wa Kanisa uliingia
maeneo mbalimbali na kusababisha maumivu kwenye Dayosisi ambapo alibainisha
kuwa Askofu Mkuu hafuati utaratibu.
Alisema watu hao ndio walitumiwa na
Askofu Mkuu kwa kutengeneza mashitaka ya Dayosisi hiyo, huku akithibitisha kuwa
maaskofu hao kutumika kukusanya saini ambapo watatu walikiri kulaghaiwa na kusaini
bila kufahamu.
Mokiwa alisema Desemba 18 mwaka jana
alikwenda kusali katika Kanisa la Ubungo ambako ilikamatwa barua pepe yenye
mazungumzo kati ya Katibu Mkuu, akiwasiliana na makundi ya Dayosisi ya Dar es
Salaam kutoa siri za ofisi.
“Kanisa la Magomeni halijawahi kushindwa
kugombana na Askofu mwingine yeyote katika Dayosisi hii, watagombana hadi na
maaskofu 27 waliobaki,” alisema.
Alisema hiyo ni roho ya vita
inayozunguka ndani yao, huku akibainisha kuundwa kwa Tume ya Askofu inayotumia
gari la Serikali namba STK 2948 mkoani Singida.
“Sisi tunafahamu Kanisa lile gari lipo
linafanya kazi za mkoa wa Singida linaingiaje kufanya kazi ya Kanisa?” Alihoji akisema
haliko kwenye mamlaka ya Kanisa.
0 comments:
Post a Comment