Kesi ya Ndama Mtoto wa Ng’ombe kutajwa leo


Grace Gurisha

MFANYABIASHARA maarufu Dar es Salaam, Hussein Ndama, maarufu kama Ndama Mtoto wa Ng’ombe (44), leo anatarajiwa kupanda kizimbani kwa mara ya nne kesi yake itakapotajwa kuangalia kama upelelezi umekamilika.

Kesi hiyo itatajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambapo awali Wakili wa Serikali, Leornad Challo aliieleza Mahakama kuwa hajui hatua ya upelelezi ilipofikia kwa sababu hakuwa na jalada la Polisi.

Pia aliieleza kuwa mawakili wanaoendesha kesi hiyo hawakuwapo kwa hiyo yeye alikuwa amewashikia tu na baada ya kudai hivyo, Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi leo na kuutaka upande wa Jamhuri ujipange kuhusu hilo, ili kusiwe na majibu ya aina hiyo tena.

Ndama anakabiliwa na tuhuma sita ikiwamo ya kutakatisha fedha haramu na kujipatia dola za Marekani 540,390 sawa na zaidi ya Sh bilioni moja kwa njia ya udanganyifu, ambapo jana alipandishwa kizimbani akiwa amefungwa pingu, jambo ambalo lilishangaza ndugu, jamaa na marafiki.

Ndama anadaiwa kuwa Februari 20, 2014 akiwa Dar es Salaam kwa nia ya kudanganya, alighushi hati ya uongo ya kuuza madini nje na sampuli ya madini, kwa kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Ltd, imemruhusu kusafirisha makasha manne ya dhahabu yenye uzito wa kilogramu 207 na thamani ya dola 8,280,000 zaidi ya Sh bilioni 16 huku akijua si kweli.

Katika tuhuma nyingine, mshitakiwa anadaiwa kuwa Machi 6, 2014 akiwa Dar es Salaam alighushi hati ya uongo kutoka ofisi za Umoja wa Mataifa, Dar es Salaam ya Machi 16, 2014 kuonesha kuwa kilo 207 za dhahabu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zilitarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru kwenda kampuni ya Trade TJL DTYL Ltd ya Australia na kwamba zilisafirishwa bila jinai yoyote.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo