Mwandishi Wetu
Felchesmi Mramba |
KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco) aliyeteuliwa kurithi nafasi ya Felchesmi Mramba,
ameanza kazi rasmi, JAMBO LEO imebaini.
Habari kutoka ndani ya makao makuu ya
Tanesco zilieleza jana kuwa Dk Tito Mwinuka ameanza kazi siku moja tu, tangu
Mramba afike ofisini hapo kwa kukamilisha makabidhiano.
“Wote wawili (Mramba na Mwinuka) walifika
hapa ofisini jana (juzi). Inaonekana Mramba alikuja kukabidhi ofisi. Sasa leo
(jana) huyo jamaa (Dk Mwinuka) ndiyo ameanza kazi rasmi,” alisema mmoja wa
wafanyakazi wa shirika hilo aliyekutana na mwandishi wa habari hizi ofisini
hapo.
Jitihada za kumtafuta Mramba azungumzie
suala hilo, ziligonga mwamba baada ya simu yake kutopatikana muda mrefu. Pia
mwandishi wa habari hii hakumpata Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo kutokana na
simu yake kuita bila kupokewa.
Ilikuaje?
Januari mosi, Rais Magufuli alitengua
uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mramba kwa kilichohusishwa
na mchakato wa kutaka kupandisha bei ya umeme.
Baada ya kumtengua, Rais Magufuli
alimteua Dk Mwinuka ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kushikilia
nafasi hiyo na kuagiza aanze kazi mara moja.
Kabla ya uteuzi huo, Rais alieleza
kushangazwa na hatua ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati, Maji na
Mafuta (Ewura) kuridhia maombi ya Tanesco kupandisha bei ya umeme kuanzia mwezi
huu, akisema jambo hilo haliwezekani na nishati hiyo haitapanda.
Katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa
la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma, Bukoba mkoani Kagera, Rais Magufuli alisema
haiwezekani apange mikakati ya kujenga viwanda halafu bei ya umeme ipande
kinyemela, bila Serikali kushirikishwa.
“Unapanga mikakati ya kujenga viwanda na
hasa katika mikakati mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme mpaka vijijini, umeme
huu unakwenda kwa watu masikini walioumbwa kwa mfano wa Mungu, halafu mtu pekee
kwa sababu ya cheo chake anapandisha kiwango hicho, haiwezekani,” alisema Rais
Magufuli.
Kauli hiyo ya Rais Magufuli ilikuja siku
moja baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuzuia
utekelezaji wa bei mpya ya umeme zilizokuwa zianze kutumika kuanzia Januari
Mosi, akisema baadhi ya taratibu zilikiukwa.
Wadau
Wakati Rais Magufuli akieleza hayo, kwa
nyakati tofauti wasomi walisema uamuzi wake huo unatokana na suala hilo la
kuongeza bei ya umeme kupingwa kila kona, kwani haiwezekani Ewura kuridhia maombi
hayo bila kupewa baraka na mamlaka za juu.
Kwa mamlaka aliyonayo, Mkurugenzi Mkuu
wa Ewura, Felix Ngamlagosi ndiye alitangaza uamuzi wa Bodi ya Ewura kupandisha
bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 8.5 badala ya asilimia 18.19 iliyokuwa
imeombwa na Tanesco.
Ewura katika agizo lake namba 16-126,
inaruhusu Tanesco kupandisha bei ya umeme kwa kiwango hicho, sambamba na
kutekeleza maagizo zaidi ya kumi, ikiwemo kuzalisha umeme kwa mitambo yenye
gharama nafuu.
Uamuzi wa Ewura kuridhia maombi ya
Tanesco uliwachanganya wananchi kutokana na kauli iliyotolewa mwaka juzi na Profesa
Muhongo kuwa kazi yake kubwa ni kuhakikisha bei ya umeme inashuka, huku
wakishuhudia Aprili mwaka jana Tanesco ikishusha bei ya umeme kwa kati ya
asilimia 1.5 na 2.4.
Hata hivyo, Oktoba mwaka jana, Tanesco
iliwasilisha maombi mapya ya kutangaza ongezeko la bei kwa maelezo kwamba
wamekuwa wakipata hasara ya Sh bilioni 40 kila mwezi, maombi ambayo Profesa
Muhongo aliyapangua, kisha kuwekwa msisitizo na Rais Magufuli.
0 comments:
Post a Comment