Leonce Zimbandu
Adam Mgoyi |
MKUU wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi, ametoa
onyo kwa wahalifu wanaochukua sheria mikononi, akisema atahakikisha wanasakwa
na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mgoyi alitoa kauli hiyo kufuatia wimbi
la wakulima kupigwa, kujeruhiwa kutiwa vilema vya maisha, akiwamo Omary Sululu
aliyepigwa panga kichwani na kushonwa nyuzi 12, tukio linalodaiwa kufanywa na
jamii ya wafugaji.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya
simu jana, Mgoyi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya
hiyo alisema atahakikisha matukio hayo yanapungua hata kwisha kabisa.
Alisema wakati mwingine taarifa
zinapotolewa inakuwa vigumu kuthibitisha kwa haraka, hivyo kutokana na matukio
yanayoendelea lazima hatua zichukuliwe.
“Matukio hayo ni mabaya na Serikali
haiwezi kuvumilia, itawasaka wahalifu waliofanya matukio hayo na adhabu
zitolewe,” alisema.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha Mamoyo,
Salehe Juma alisema wanashangaa viongozi kuendelea kuwatia moyo huku ndugu zao
wakiendelea kupigwa na wafugaji bila hatua kuchukuliwa.
Alisema wakati huo wa matukio, viongozi
wengi hupenda kutoa kauli za kuonesha wako pamoja na wakulima, lakini baada ya
msimu huo kupita, mikakati inayoratibiwa haisimamiwi tena.
“Tunahitaji ufuatiliaji na hatua
zichukuliwe kwa wahusika ambao wanajichukulia sheria mikononi kupiga na kujeruhi
wakulima kwa vile wanazuia mifugo isile mazao yao,“ alisema.
Alisema umefika wakati wakulima wanafikiri kwa vile wanaopigwa si ndugu za
viongozi ndiyo maana hakuna hatua za haraka zinachukuliwa.
0 comments:
Post a Comment