Salha Mohamed
Angela Kairuki |
MKOA wa Dar es Salaam umetajwa kuongoza
kwa kuwa na kaya masikini hewa chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf)
ukifuatiwa na Mwanza.
Kaya hizo 5,000 ni kati ya 55,692 hali
inayosababishwa na wakazi wengi kuwa mkoani humo.
Hayo yalibainishwa juzi na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, wakati
akizungumza kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha ITV.
“Lakini tunaamini hapa ndipo penye wakazi
wengi, hivyo ni dhahiri kwamba wengi watatoka mkoa huo, ukifuatiwa na Mwanza,” alisema.
Alisema bado uhakiki wa kaya unaendelea,
watakapomaliza takwimu hizo zinaweza kubadilika.
Alisema kutokana na hali hiyo, kuna watu
walihusika kutumia fedha vibaya hizo ikiwa ni pamoja na wananchi kufunguliwa kesi
huku akibainisha kuwa kila mhusika atafuatwa ili kurudisha fedha hizo.
“Lazima waliohusika kuchukua fedha za
Tasaf kwa namna moja au nyingine wazirudishe…wapo ambao wameanza kuzirudisha,” alisema.
Kairuki alitaka wananchi kutoa taarifa
na kufanya uhakiki wa kaya masikini, ili kusababisha wasiostahili kunufaika na
mpango huo kutosajiliwa.
Alisema wananchi wanapaswa kushiriki
mchakato wa kujua kaya masikini ili kuhakikisha inapatikana orodha inayokidhi
vigezo.
“Tunawaomba washiriki li tupate orodha
ambayo kweli inakidhi vigezo vya umasikini kama vilivyowekwa na ofisi yetu ya
Taifa ya Takwimu,” alisema.
Alisema mara ya mwisho walikuta kaya 5,500
huku akibainisha kuwa kwenye mkupuo wa malipo watatoa wanufaika wengi zaidi
wasiohusika.
“Serikali imepoteza Sh bilioni 6.4 kwa
kaya zisizokusudiwa, tutakapofanya malipo mwezi huu tutapata hesabu nzuri zaidi,
kwani wasiokuwa wanufaika wameshatolewa,” alisema.
Alisema hakuna mtumishi atakayeachwa ikithibitika
alihusika kuchukua fedha za Tasaf.
“Serikali hatuwezi kufumbia macho hata
kama ni asilimia chache zilizochukuliwa hizi ni za masikini, aweze kumsaidia na
kupata huduma nzuri.
“Tulishauriana na Waziri wa Tamisemi,
George Simbachawene wakasimamishwa waratibu katika halmashuri za wilaya 91,
utumishi tulisimamisha takribani 113 ambapo washauri 106 na maofisa wengine
Tasaf makao makuu,” alisema.
Alisema waliwasimamisha ili kupisha uchunguzi
ambapo kwa sasa wameunda kamati ya uchunguzi ambapo ikithibitika hatua
zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema watendaji wa vijiji hawastahili
fedha hizo kwani hawana vigezo vya umasikini.
Aliongeza kuwa kuna changamoto ya watu
kutokuwa wawazi wanapoulizwa undani wa maisha yao kwa kuona wanadhihakiwa.
Kairuki alisema wapo waliokuwa wakidhani
kuwa fedha hizo ni za Freemason na kushindwa kuzichukua.
0 comments:
Post a Comment