Hajji Kameta, Daystar na Peter Akaro
Mwita Waitara |
SIKU chache baada ya wananchi wa Magole
‘A’ Kivule kuvunjiwa nyumba, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara amemshutumu Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda kwa kukaa kimya, huku akimwomba Rais John Magufuli
kutekeleza mambo makuu mawili ili kutatua mgogoro huo.
Akizungumza Dar es Salaam juzi kwenye mkutano
wa hadhara na wananchi hao, Waitara alisema Makonda anaufahamu mgogoro huo
tangu akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na aliyemkabidhi ofisi ni Jordan Rugimbana
baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
“Kwa hiyo walifanya makabidhiano ya
ofisi na suala hili lilikuwepo pia, kama walikabidhiwa kuwa hakikisha kuwa watu
wa Magole wanapingwa, wanavunjiwa nyumba na asiende kuwasikiliza, hayo ndiyo
yalikuwa makubaliano vinginevyo alipaswa awe amekuja hapa,” alisema Waitara.
Aliongeza: “Lakini sasa Makonda amekuwa
Mkuu wa Mkoa hivyo yeye na Rugimbana wanazungumza kauli moja, huenda hadi sasa
wanapigiana simu kuhusu jambo hili.”
Mbunge huyo alisema anaamini hivyo, kwa
sababu kama Makonda alitoka ofisini kwake na msafara wa magari zaidi ya 30
kwenda Gongo la Mboto kumwuliza Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa mapato na
matumizi wakati Halmashauri haijawahi kumpa fedha yoyote, jambo ambalo ni dogo,
iweje ashindwe kufika walipovunjiwa nyumba wananchi wake kwa mamia.
“Na mtu ambaye angepaswa kuondoa utata kwa
kusema ni Ilala ua Temeke ni Mkuu wa Mkoa, kwa sababu anahusika na wilaya zote,
lakini hajafika. Wanaosema nyie ni wa Temeke mbona hadi sasa hawajafika
kuwasaidia?” Alihoji.
Aliongeza kuwa hadi sasa hakuna kiongozi
wa ngazi ya mkoa ambaye amewahi hata kupiga simu kuulizia hali ya waathirika
hao au kutoa pole.
Katika hatua nyingine, Waitara alisema
amepata taarifa za chini kwa chini kuwa Rais Magufuli anafuatilia mgogoro huo
kwa kutuma watu wake kutafuta taarifa za eneo hilo.
“Namwomba Rais Magufuli mambo mawili;
kwanza, atambue hapa kuna matumizi mabaya ya madaraka kwa watu alioteua, kama
alitaka kujua angekuja kwa sababu aliowatuma wana maslahi na eneo hili.
“Rais kwa kuwa amekuwa akifika maeneo
kwa kushitukiza na kama kuna jambo muhimu Dar es Salaam ambalo anatakiwa kulitumbua
majipu na kushitukiza ni hapa Magole Kivule, akifanya hayo mambo mawili atakuwa
amewatendea haki Watanzania na masikini wa nchi hii,” alisema Waitara.
Alisema ni vema Rais atambue kuwa
wananchi wa Kivule wamekuwa waathirika, kwa sababu wao ni masikini na hawajui
sheria, hivyo hahitaji kwenda mikoani, anzie na Dar es Salaam ambako pia kuna
watu wanaonewa.
Aliongeza kwamba anafahamu kuwa mgogoro
huo ulitengenezwa kwa sababu Rugimbana alikuwa Mwenyekiti wa UVIKIUTA kipindi
cha nyuma na walikwenda kwa Mwalimu Julius Nyerere (marehemu) kuomba eneo la
kulima na kupewa na ndilo lina utata.
“Lakini hawataki kusema eneo lina ukubwa
gani, pia baada ya umri kwenda, Rugimbana amejigeuza kuwa mlezi wa UVIKIUTA na
aliwahi kuhojiwa na Mahakama ya Ardhi Temeke kuhusu eneo hili,” alisema.
Waitara aliwaeleza wananchi hao kuwa
wameamua kuachana na wakili aliyekuwa
anasimia suala hilo mahakamani, kwani ameshindwa kuomba pingamizi wakati sheria
zinaruhusu, amekaa kimya.
Awali mjumbe wa Kamati iliyokusanya
misaada kwa ajili ya waathirika, Eliudi Mosire alisoma risala fupi iliyosema
kuwa wananchi wengi hawana malazi, makazi, chakula na usalama wao na mali zao ni
mdogo.
Wakati akiendelea kusoma risala hiyo,
vilio vya akina mama vilisikika mbele ya mbunge wao.
Mosire alisema nyumba zilizovunjwa ni
760, ambazo zilikuwa zikihifadhi watu 540 na sasa kaya 320 hazina pa kuishi,
huku kaya 220 zikihifadhiwa kwa ndugu na jamaa.
Kutoka na hali hiyo, watu mbalimbali
pamoja na Mbunge walichanga fedha, unga, mafuta, sabuni, sukari na nguo kwa
ajili ya kaya 136 ambazo inaelezwa zipo kwenye hali mbaya zaidi.
Maoni
Mkazi wa eneo hilo, Mwanaisha Hamisi alimwomba
Rais Magufuli kutembelea eneo hilo na kushuhudia shida wanayopata kwa sasa.
“Aliangalie suala hili, asisikilize
maeneo ya kuambiwa, kwa sababu watu wana hali mbaya, tangu tulipovunjiwa watu
wanalala nje, watoto hawaendi shule na wengine wamejifungua na hawana sehemu ya
kuishi,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Abduly
Majengo alimpongeza Mbunge huyo kwa kuwaletea misaada, kwani hakuna kiongozi
mwingine wa ngazi za juu aliyewaletea misaada.
Asha Mgae alisema licha ya misaada waliropewa
na Mbunge, hawaelewi kama wataendelea kuishi katika eneo hilo au watahama.
“Angetakiwa atuweke wazi kabisa, kama
tunahama au tutaendelea kuishi hapa, kwa sababu unaweza kujenga chumba kimoja
wakavunja tena, mimi sijamwelewa,” alisema.
Ujumbe
Katika mkutano huo, wananchi walibeba
mabango yenye ujumbe mbalimbali kuhusu tukio hilo.
Baadhi ulisomeka: ‘Bora kuishi na nyoka
ndani kuliko Rugimbana’, ‘Polisi TMK wezi tu’, ‘Rais Magufuli upo au umesafiri?’
0 comments:
Post a Comment