Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA) imekamata mkazi wa Temeke (jina linahifadhiwa) akiwa na lita 520 za
mafuta ya taa yanayodaiwa kuibwa kwenye mabomba kwenye bandari ya Dar es
Salaam.
Taarifa kutoka Mamlaka hiyo zilieleza
kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa hivi karibuni akiwa kwenye mtaro unaopokea maji
machafu kutoka baharini, akiwa na madumu 13 yenye ujazo wa lita 40 kila moja.
“Askari wa TPA waliokuwa doria ndio
waliomkamata. Mtu huyo alitoboa moja ya mabomba ya mafuta ya kampuni mbalimbali.
“Askari pia walikamata vifaa vya uhalifu kama nyundo, tindo,
bisibisi, visu, tochi ndogo 10 na mpira wa kunyonyea mafuta kutoka kwenye mabomba
makubwa,” zilieleza taarifa hizo.
Zilieleza kuwa viongozi wa kampuni za
usambazaji mafuta ambazo mabomba yao yamepita eneo hilo walijulishwa kuhusu wizi
huo ili kuchunguza na kujua mafuta hayo ni ya kampuni ipi.
“Kwa sasa eneo husika liko chini ya uangalizi
wa askari wa kikosi cha Polisi Bandari wakati uchunguzi zaidi wa tukio hili
ukiendelea ili kubaini mtandao unaohusika,” taarifa zilifafanua.
Hivi karibuni Mamlaka hiyo iliimarisha
ulinzi wa Bandari hiyo ikiwa ni pamoja na kufunga mitambo ya kamera (CCTV).
0 comments:
Post a Comment