Suleiman Msuya
Maalim Seif |
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema
taarifa zinazosambazwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kwamba Katibu
Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad anataka kuhama chama hicho ni za kupuuzwa kwa kuwa
hazina ukweli.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor
Ahmed Mazrui alisema hayo jana alipozungumza na JAMBO LEO baada ya baadhi ya
vyombo vya habari kuripoti kuwa Maalim atataka kuondoka ndani ya chama hicho
cha upinzani.
Alisema tangu kuibuka kwa mgogoro ndani
ya CUF na Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba imekuwapo mikakati ya
kuwakatisha tamaa jambo ambalo halitafanikiwa.
Mazrui alisema wanaopanga mikakati
wamehangaika kila njia na wameonekana kukwama, hivyo kuibuka na mkakati wa
kumzushia Katibu Mkuu kuhama chama.
“Hivi unafikiria Katibu Mkuu anaweza
kuhama chama katika mazingira rahisi kiasi hicho? Hiki chama amekipigania vya
kutosha wataondoka wao,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwataka wana
CUF kuendelea kutoa ushirikiano kwa Katibu Mkuu wao na kupuuza kauli za watu
ambao wamepoteza mwelekeo kisiasa.
Alisema CUF si chama kinachotegemea mtu
mmoja, na pia hakiko tayari kumpoteza Maalim kwa vibwagizo vya vibaraka wa
chama tawala, ambao hawataki kupigania mabadiliko nchini.
Aidha, kuhusu chama kuwa kimya kuhusu
madai yao ya ushindi katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana, alisema bado
wanaendelea na mchakato huo na watatoa taarifa hivi karibuni kuhusu hatua
waliyofikia.
Mazrui alisema kila kitu kinakwenda
vizuri na kutaka wana CUF kuwa na subira katika kipindi hiki, kwani mambo
mazuri hayahitaji haraka.
Alisema ushirikiano wanaopata kutoka
jumuiya ya kimataifa ni mzuri hali ambayo inawapa matumaini ya kuhakikisha kuwa
haki inapatikana.
“Suala la madai ya ushindi wa uchaguzi
linakwenda vizuri, na naamini hatima yake itapatikana kwa busara, ni vema wana
CUF kuwa na subira,” alisema.
Jana katika baadhi ya magazeti
ziliandikwa habari zikimhusisha Maalim na kuhama CUF na kutajwa kutarajia
kuhamia vyama vya ADA-TADEA, AFP au ACT-Wazalendo, ambapo viongozi wa vyama
hivyo walikanusha taarifa hizo.
Hali kadhalika Katibu Mkuu huyo alihusishwa
na kutaka kujiunga na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
0 comments:
Post a Comment