Suleiman Msuya
TAASISI ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)
yaitesa TRA. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na taarifa ya mizigo ya
taasisi hiyo kudaiwa kuzuiwa bandarini hadi ilipe kodi, kuandikwa na vyombo
mbalimbali.
Siku chache baada ya Ikulu kukanusha
taarifa hizo zilizodai Rais John Magufuli anahusika kuzuia mizigo hiyo, Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), imesisitiza kuwa taarifa hizo hazikuwa za kweli.
Kupitia Kamishna Mkuu, Aliphayo Kidata
jana TRA ilikanusha taarifa hizo ikisema orodha iliyochapishwa na baadhi ya
magazeti nchini ikijumuisha jina la WAMA haikuwa sahihi.
Kidata alisema WAMA iliingiza nchini makasha
11 ya vitabu na kamusi kutoka Japan kwa ajili ya matumizi ya elimu.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya
Afrika Mashariki ya 2004, pamoja na
Sheria ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2015 vitabu hivyo havitozwi kodi
ya forodha wala VAT,” alisema Kidata.
Alisema vitabu hivyo vilitozwa tozo ya
uondoshaji mizigo bandarini Sh 42,483 na ya Maendeleo ya Reli Sh 106,438 ikiwa
ni jumla ya Sh 148,921.
“Baada ya malipo hayo kufanyika, vitabu
hivyo vilichukuliwa na WAMA tangu Agosti 10,” alisema.
Alisema taarifa zilizoandikwa na baadhi
ya magazeti hivi karibuni juu ya vitabu hivyo kuwa kwenye orodha ya bidhaa zinazopaswa
kupigwa mnada kwa sababu ya kutolipiwa kodi haikuwa sahihi.
Kamishna huyo alisema vitabu hivyo
havikupaswa kutozwa kodi ya forodha wala VAT kwa mujibu wa sheria, hivyo WAMA haikupaswa
pia kuomba msamaha wa kodi kwenye mamlaka yoyote.
Desemba 4 Ikulu kupitia Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais ilitoa taarifa za kukanusha Rais Magufuli kuhusika kuzuia
mizigo hiyo bandarini mpaka hapo itakapolipiwa kodi.
“Tunapenda kuutarifu umma kuwa taarifa
hizo si za kweli na ni uzushi, kwani Rais Magufuli hajawahi kuzuia wala kuagiza
kuzuiwa kwa mizigo ya Mama Salma Kikwete,” ilisema taarifa.
Taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli alisikitishwa
na uzushi huo unaofanywa kwa lengo la kumchafua Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na
familia yake.
“Nimesikitishwa sana na uzushi unaofanywa
dhidi ya Rais mstaafu Dk Kikwete na mke wake Mama Salma, tafadhali
mnaotengeneza uzushi huu acheni mara moja na mwacheni Rais mstaafu Kikwete
apumzike,” ilisema taarifa hiyo.
“Rais mstaafu Kikwete amefanya kazi
kubwa ya kulitumikia Taifa hili, amestaafu anapumzika, narudia mwacheni
apumzike, Serikali haitaendelea kuvumilia uzushi na uchonganishi huu unaofanywa
kwa makusudi ili kuchafua viongozi wastaafu,” Rais Magufuli alikaririwa akionya.
0 comments:
Post a Comment