Kairuki ataka maofisa TASAF wasimamishwe


Abraham Ntambara

Angella Kairuki
WAZIRI wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwasimamisha kazi maofisa washauri na ufuatiliaji 106 kwenye halmashauri walioshindwa kufuatilia na kusimamia Mpango huo.

Aidha, amemtaka kuwasimamisha maofisa watano wa makao makuu wanaosimamia mpango huo pamoja na Meneja wa Uratibu na Mkurugenzi wa Uratibu ambao ndio viongozi wasimamizi wao wakuu.

Waziri Kairuki alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF kuhakikisha uchunguzi unakamilika katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja kuanzia jana.

“Naagiza ufanyike uchunguzi wa kina ili kubaini ushiriki wa maofisa hao na kuchukua hatua stahiki kwa watakaothibitika kuhusika na usimamizi, ufuatiliaji na uwajibikaji,” alisema Kairuki.

Aliongeza kuwa kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI tayari ameelekeza waratibu wa TASAF wa Wilaya wasimamishwe kazi na uchunguzi wa jinsi walivyojihusisha kuvuruga utekelezaji wa Mpango huu, hadi kuandikisha kaya zisizo na sifa.

Aliitaka TASAF makao makuu waendelee kushirikiana na halmashauri kuongeza udhibiti wa fedha wa malipo na kuhakikisha fedha zinalipwa kwa kaya zenye sifa, ambapo anayelipwa atalazimika kuwasilisha vitambulisho visivyopungua viwili.

Waziri Kairuki alifafanua kuwa vitambulisho hivyo ni pamoja na cha Mpango na kitambulisho kingine kinachotambulika na Serikali kama cha mpiga kura na cha Taifa ili kuwa na uhakika kuwa fedha zinalipwa kwa mhusika sahihi.

Aliielekeza TASAF makao makuu kuendelea kushirikiana na halmashauri zote kukamilisha uhakiki wa nyumba kwa nyumba katika halmashauri nchini kabla ya malipo yanayofuata kati ya Januari na Februari.

Aidha, alisisitiza kuwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri, majiji, manispaa, miji na wilaya wahakikishe fedha  zilizotolewa kwa kaya zisizo na sifa zinarejeshwa ili zinufaishe wengine.

Pia alitoa rai kwa watumishi wa TASAF na wa halmashauri wanaohusika na mpango wa TASAF kuwa waaminifu, waadilifu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma pamoja na zile zinazosimamia mpango huo na kwamba Serikali haitawavumilia wa kusita kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayekiuka Taratibu zilizowekwa za Mpango huo.

Aidha, alisema baada ya uhakiki kufanyika kaya 55,692 zeliondolewa kwenye Mpango kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kaya kuhama kijiji/mtaa, kutojitokeza mara tatu mfululizo kupokea msaada, vifo na kaya zingine kukosa sifa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo