Sharifa Marira
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA) inatarajia kutumia Sh bilioni 132 kukarabati bandari ya Dar es Salaam kwa
kuboresha miundombinu ili iweze kupokea mizigo mingi.
Ukarabati huo utasaidia kuiinua Bandari
hiyo inayopokea mizigo inayoingia nchini kwa asilimia 90 hadi 95 ukitokana na
msaada wa fedha kutoka Serikali ya Uingereza kupitia Taasisi ya Trade Mark East
Africa (TMEA).
Hatua hiyo inatajwa kumsaidia Rais John
Magufuli kufikia malengo yake kuinua uchumi wa Taifa na kuwa nchi ya kipato cha
kati, kutokana na ukweli, kwamba baada ya ukarabati huo Bandari hiyo itakuwa na
uwezo wa kuchukua mizigo mikubwa zaidi ya bandari zingine za nchi jirani.
Kwa mujibu wa TPA, kazi ya ukarabati inatarajiwa
kuanza mara moja baada ya jana kusaini mkataba wa makubaliano na Taasisi ya
Trade Mark East Afrika (TMEA) tawi la Tanzania.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba
huo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema ukarabati huo ni mkubwa
na lango lote la Bandari litafumuliwa na kazi hiyo itakamilika ndani ya miaka
minne ijayo.
Alisema kwa sasa wanapitisha meli za
tani milioni 15, lakini baada ya uboreshaji huo watapokea meli za tani milioni
26.
“Tumetafuta wakandarasi na kuna Mchina
anaonekana kushinda, kama akipita tutaanza mradi mara hivyo itakwenda haraka na
itakuwa nzuri, ikifika mwaka 2019 na 2020 tuna imani kila kitu kitakuwa sawa,” alisema
Kakoko.
Alisema baada ya uboreshaji, TPA
itaendelea kuboresha bandari zingine ikiwamo ya Bagamoyo ili kusaidiana na ya
Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa TMEA Tanzania, John Ulanga
alisema fedha hizo si mkopo bali ni msaada kwa Serikali na endapo mradi huo
utakwenda vizuri na kukamilika mwaka 2019 kuna uwezekano wa kuomba fedha kwa ajili ya bandari zingine
ikiwamo ya Kigoma.
Alisema TMEA wana miradi mingi ya kuboresha
mazingira ya kibiashara na wanaboresha bandari hiyo kutokana na umuhimu wake,
kwani asilimia 40 ya kodi inapatikana kupitia bandari hiyo.
“Tunaishukuru Uingereza ambayo imetoa
msaada huu na kupitia kwetu tumeleta hapa TPA katika mradi huu mkubwa ambao
utaleta mabadiliko chanya ya kushindana na bandari zingine ikiwamo ya Mombasa, Kenya,”
alisema Ulanga.
0 comments:
Post a Comment