Hajji Kameta, Daystar
Ali Hassan Mwinyi |
RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi ameongoza
mamia ya wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kwenye maziko ya aliyekuwa daktari
wake, Profesa Idrisa Mtulia ambaye alifariki dunia nyumbani kwake juzi.
Pamoja na Mwinyi, walikuwapo pia Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Kingunge Ngombale-Mwiru, Adam Malima na Mbunge
wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete.
Wengine ni Waziri Mkuu wa zamani Edward
Lowassa, Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yussuf Masauni na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya.
Akizungumza kwenye maziko hayo Shekhe wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema Mtulia alikuwa kiongozi mcha
Mungu hivyo ni vema kila mwanadamu akaishi kwenye misingi hiyo.
Shekhe Mussa alisema ni vema kila mtu
akajiandaa kwa kifo, kwani kinakuja bila taarifa hivyo ni vema kufanya ibada
ili kuvuna mema ahera.
Kinana amemtumia salamu za rambirambi
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Pwani, Mwishehe Mlao akisema marehemu alikuwa mmoja
wa wanachama waliotumikia chama na Serikali kwa uadilifu wa hali ya juu, akiwa
pia Mwenyekiti wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Profesa Mtulia alipata kuwa Katibu Mkuu
wa Wizara ya Maji na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kuanzia
mwaka 2002 hadi 2007. Ameacha mjane na watoto sita.
0 comments:
Post a Comment