Walimu jela miaka 20 kwa wizi wa mitihani


*Mmoja alidanganya askari wakampa ufunguo
*Wadakwa wakigawia karatasi wanafunzi 15

Costantine Mathias, Simiyu

WALIMU wawili wa sekondari za Nyawana na Shishani wilaya ya Bariadi na Itilima mkoani hapa wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kwa kosa la kuiba na kuvujisha mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.

Walimu waliohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, ni Issa Makene (40) wa sekondari ya Shishani na Solela Mangura (26) mwalimu wa kujitolea wa sekondari ya Nyawana, ambaye hata hivyo hakuwa mahakamani wakati hukumu ikitolewa jana kutokana na kuruka dhamana na kutokomea kusikojulikana tangu kesi yake itajwe mwaka 2013.

Awali akiwasomea mashitaka yao katika kesi namba 176/2015, kabla ya hukumu kutolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, mwendesha mashitaka wa serikali, Moses Mafuru alidai tukio hilo lilitokea Novemba 10, 2013, katika sekondari ya Sagata.

Mafuru alidai kuwa Mwalimu Makene akiwa Mkuu wa Kituo cha Mitihani cha sekondari ya Sagata, siku ya tukio wakati wa chakula cha usiku aliwalaghai askari waliokuwa wakilinda mitihani katika kituo hicho.

Aliendelea kudai kuwa Makene aliwaomba askari hao wampe ufunguo wa chumba kilichohifadhi mitihani hiyo na baada ya kupewa, alifungua chumba na kwenda moja kwa moja kwenye kabati lenye mitihani hiyo.

Mafuru alidai kuwa mara baada ya kufungua kabati mtuhumiwa, alichukua bahasha lenye mtihani wa somo la Fizikia kisha kwenda kuuficha chini ya uvungu wa kitanda chake shuleni hapo.

Alidai kuwa kesho yake baada ya mwalimu huyo kuchukua bahasha Novemba 11, 2013 aliichana na kutoa karatasi moja ya mtihani huo na kumkabidhi mwalimu Solela.

Halikadhalika, walimu hao walikuwa kwenye harakati za kuwapa wanafunzi 15 wa shule hiyo ambao mwendesha mashitaka aliwataja   kuwa ni Abasi Makwaya, Veronica Jonathan, Mboji Masike, Saka Masuki, Milembe Mabula, Makula Saya na Prisca Jonathan.

Wengine ni Getruda Senga, Buye Masike, Msafiri Samson, Japhet Martine, Alex Jackson na Khamis Nkwabi.

Akisoma hukumu, Hakimu John Nkwabi aliamuru washitakiwa hao kwenda jela miaka 20 kila mmoja, kwa kuwa Mahakama ilijiridhisha na ushahidi ulitolewa na upande wa mashitaka.

Kuhusu hukumu hiyo, Ofisa Elimu wa Mkoa, Julius Nestory alisema haki imetendeka na kuwa fundisho kwa walimu wengine, huku akibainisha kuwa hajafurahia kufungwa kwa walimu hao.

Aliwataka walimu hao kukata rufaa kama wanaona hawajatendewa haki, huku akiwataka wengine kuwa na nidhamu kazini kwa kufuata sheria na kanuni za utumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na wanaopangiwa kusimamia mitihani kuachana na vitendo hivyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo