Watakiwa kujihadhari na kipindupindu


Ally Daud wa MAELEZO

Ummy Mwalimu
MIKOA na halmashauri nchini zimetakiwa kuweka hadhari ya kipindupindu kwa kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira hasa wakati wa mvua za vuli na msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ili kuepuka ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa jana Dar es Salaam, na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa kipindupindu kwa Novemba.

Waziri Ummy alisema mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo ishirikishe sekta za afya bila kusahau jamii na kuhakikisha kila halmashauri inaunda na kuimarisha Kamati ya Afya ya Kata.

Aliiagiza mikoa na halmashauri zote nchini kutoa taarifa ya wagonjwa wapya wa kipindupindu ili jitihada za makusudi za kupambana na ugonjwa huo zifanyike mapema ili kujenga Taifa lisilo na magonjwa ya mlipuko.

Alisema takwimu zinaonesha kuwa Novemba mikoa sita ilikuwa na wagonjwa ambayo ni Morogoro 282, Dodoma 96 na vifo 2, Mara 31, Kigoma 30 na vifo 4, Arusha 11 na Dar es Salaam 8 kutoka wagonjwa  250 na vifo 4 kwa Oktoba.

Wakati huo huo, Waziri Ummy alipokea vifaa vya matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi vyenye thamani ya takribani Sh milioni 100 za kitanzania kutoka shirika la kimataifa la Pink Ribbon Red Ribbon ili kupambana na ugonjwa huo nchini.

Akikabidhi msaada huo, Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Celina Schocken alisema walitoa vifaa hivyo ili kuisaidia nchi juhudi zake za kupambana na saratani ili kuokoa maisha ya wanawake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo