Leonce Zimbandu
Zitto Kabwe |
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimemshauri Rais
John Magufuli kuunda kitengo cha huduma za chini za uendeshaji wa viwanja vya
ndege, badala ya kuvibinafsisha.
Huduma hizo ni utunzaji wa mizigo,
abiria, mfumo wa kompyuta, usafirishaji na upokeaji mizigo na usafiri wa mabasi
kutoka na kwenda uwanja wa ndege.
Zingine ni mfumo wa usalama wa viwanja,
kitengo cha uhandisi cha kukarabati ndege zinazoharibika na huduma ya kuuza
mafuta isiwe lazima zipewe kampuni za Puma au Oilcom.
Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Anna
Mghwira alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.
Alisema lengo la kuboresha sekta ya anga
iwe ni kurudishia Shirika la Ndege la Taifa (ACTL) mamlaka ya kumiliki huduma
zote za chini za uendeshaji wa viwanja vya ndege.
“Ni vema huduma za chini zikaimarishwa
haraka, kabla ndege zingine nne kuwasili nchini, kwa vile huduma hizo ni vitega
uchumi vya mashirika yote ya ndege
duniani, ACTL itapata fedha nyingi ikisimamia huduma hizo,” alisema.
Alisema anashangaa Tanzania kwenda
kinyume na utaratibu unaotumiwa na mataifa mengine ambayo viwanja vya ndege
vinamilikiwa na wananchi Wazalendo.
Aliongeza kuwa utaratibu wa kimataifa
unataka mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege umilikiwe na Wazalendo
walioajiriwa kwenye mamlaka hiyo, ili kulinda usalama wa viongozi.
Aidha, Mghwira alisema udhaifu wa
viwanja vya ndege ulianza mwaka 1990 baada ya viongozi kujihusisha na ufisadi
wa kuuza mali za umma kwa wageni bila kujali usalama wa nchi.
Alisema mashirika matano hayakupaswa
kubinafsishwa, likiwamo ATC, Wakala wa Meli Tanzania (NASACO) na Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco).
Mengine ni Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Shirika la Simu Tanzania
(TTCL), ubinafsishaji huo ulifanyika kwa kuzingatia rushwa ya asilimia 10,
kwamba hiyo ni aibu ya kudumu Tanzania.
Katika kipindi hicho, alisema shirika
hilo lilianza kuyumba baada viongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi,
Idara ya Anga kuuza njia za ndege kwa mashirika mengine na kuingia mikataba
mibovu.
0 comments:
Post a Comment