Suleiman Msuya
Dk Vincent Mashinji |
KATIBU Mkuu wa CHADEMA, Dk Vincent
Mashinji, amesema changamoto wanazokutana nazo katika kufanya siasa zinatokana
na upofu wa viongozi wanaowazuia.
Wakati Mashinji akieleza hayo, Mwenyekiti
wa Chama hicho, Freeman Mbowe ameanza ziara ya kikazi ya siku 14 Ulaya kuwakilisha
chama kwenye Mkutano Maalumu wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani.
Akizungumza jana na JAMBOLEO, Mashinji
aliweka bayana kuwa pamoja na zuio la mikutano ya hadhara, bado wapo watendaji na
viongozi wasiojiamini hivyo kubana demokrasia.
Mashinji alisema moja ya mikakati yao
kipindi hiki ni kufanya siasa za kujenga chama kimfumo na kuachana na siasa za
kiuanaharakati hivyo uamuzi huo wa kuwazuia haujaathiri jambo lolote kichama.
“Yapo mafanikio makubwa sana kutokana na
mfumo wa siasa ambazo tunazifanya na zimeanza kusumbua watawala, hali ambayo
inasababisha kila kukicha wanaibuka na mikakati mipya ya kukabiliana nasi,”
alisema.
Katibu Mkuu huyo alisema siasa ni
mchakato unaokutana na vikumbo vingi, hivyo wao wamejipanga kukabiliana navyo
hatua kwa hatua.
Alisema jambo la kupongeza ni wananchi
wamewaelewa watawala kuwa ni watu wa aina gani, hivyo hawapati shida ya kufanya
nao kazi za kila siku.
Mashinji alisema kila kukicha wanabuni
mbinu mpya ya kufikia wananchi na kuwafikishia ujumbe, hivyo mikakati ya
Serikali na chama kuwakabili haiwezi kufua dafu.
“Unajua mikutano ya ndani imekuwa ikitoa
matokeo chanya kwa wanachama wetu, hivyo naamini ikiendelea hivi hivi ni hatua
nzuri katika chama,” alisema.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani,
vyama vya siasa nchi vimekuwa katika hali ngumu ya kufanya siasa, hali ambayo
imekuwa ikiibua malalamiko kutoka pande mbalimbali za nchi, huku wengine
wakiona kama ni mkakati wa Serikali kuua vyama vya upinzani.
Katika matamko na kauli za viongozi wa
Serikali wakiongozwa na Rais, wamekuwa wakisema waachwe wafanye siasa na siasa
zitaanza mwaka 2020 jambo ambalo ni kinyume na Katiba na Sheria ya Vyama vya
Siasa, ambayo inataka vyama vifanye siasa.
Katazo hilo limesababisha wanachama na
viongozi wa vyama vya siasa wakizuiwa kufanya mikutano na wengine kushikiliwa
na Polisi kwa muda ambapo kwa siku za karibuni, hali hiyo ilimkumba Katibu Mkuu
wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na baadhi ya viongozi wa Chadema.
Kwa upande mwingine, Msemaji wa Chadema,
Tumaini Makene alisema Mbowe anaongoza wajumbe wa chama hicho kwenye mkutano huo
ambamo atapata nafasi ya kuhutubia.
Alisema katika ziara hiyo yumo
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mawasiliano,
John Mrema na utazuru pia Ujerumani, Uingereza na Ubelgiji yaliko Makao Makuu
ya Jumuiya ya Ulaya (EU).
Makene alisema akiwa London, Mbowe na
ujumbe wake watakutana na viongozi wa Serikali, wabunge, ujumbe maalumu wa
Jumuiya ya Madola na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za kimataifa.
“Mjini Brussels (Ubelgiji), atapata
fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na viongozi wa EU na taasisi zake,” alisema.
Makene alisema wajumbe kutoka nchi
mbalimbali watazungumza na kubadilishana uzoefu kuhusu demokrasia, mafanikio na
changamoto katika maeneo yao na dunia kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment