Grace Gurisha
Tundu Lissu |
KESI ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), imeanza kusikilizwa kwenye Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa polisi kukiri kutomkamata kiongozi huyo
kutokana na wadhifa alionao.
Askari namba E 4128 Ndege alikiri jana
mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa wakati akitoa ushahidi dhidi ya Lissu,
kuwa Juni 28 kwenye viwanja vya Mahakama hiyo alishindwa kumkamata akitoa
maneno ya uchochezi, kwa sababu ni kiongozi, kwa hiyo walitumia busara.
Alidai maneno hayo ni: “Mamlaka ya
Serikali mbovu ya kidikteta uchwara, inapaswa kupingwa kwa nguvu zote na kila Mtanzania
na kwamba kama nchi itaachwa katika utawala wa kidikteta, itaingia katika giza
nene.”
"Kisheria Mrakibu Msaidizi wa
Polisi Kimweri naye alikuwa na mamlaka ya kumkamata Lissu kutokana na maneno
yake ya uchochezi, lakini kutokana na wadhifa alionao kwa kuwa kiongozi, tulitumia busara ili apatikane sehemu
nyingine," alidai Ndege.
Alidai kuwa baada ya kutoa taarifa hiyo
kwa viongozi, walichukua hatua ya kumkamata nje ya eneo ambalo alitolea maneno
hayo ya uchochezi.
Pia alidai kuwa si lazima mtu anapofanya
kosa akamatwe papo hapo, kwa sababu inategemea na kosa lenyewe, kwa mfano mtu
anaweza kutukana akaachwa kwa sababu ndani ya tusi husika hakuna uzito.
Akijibu maswali ya upande wa utetezi,
Ndege alidai tangu Lissu atamke maneno hayo, hajawahi kusikia yamesababisha uvunjifu wa amani na pia hajawahi kupokea
malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu maneno hayo.
Katika kesi hiyo, inadaiwa kwa nia ya
kushawishi na kufanya uchonganishi kati ya wananchi wa Tanzania na Serikali,
Lissu alitoa maneno ya uchochezi.
0 comments:
Post a Comment