Mama Maria Nyerere apongeza Serikali

Mwandishi Wetu

Mama Maria Nyerere
MJANE wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere, ameipongeza Serikali kwa namna inavyotoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu chini ya mpango wa elimu bure, hivyo kuongeza nafasi na hadhi ya mwanamke katika jamii.

Mama Maria alitoa pongezi hizo kwenye mahojiano maalumu kuhusu maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam jana. 

“Elimu imebadili nafasi ya mwanamke katika jamii, tukiangalia wakati tunapata uhuru wanawake wengi walikuwa bado hawajui kusoma na kuandika,” alisema Mama Maria.

Aliongeza kuwa wakati Tanzania ikipata Uhuru mwaka 1961 idadi ya wanawake walioshika nafasi za uongozi walikuwa wachache na hazikuwa nafasi kubwa, jambo ambalo ni tofauti na sasa, kwani kwa mara ya kwanza Tanzania ina Makamu wa Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan.

Alisema pamoja na changamoto zilizopo, Serikali za awamu zote zilijitahidi kuhakikisha zinapiga hatua za kukabiliana na adui ujinga.

Kwa mujibu wa Mama Maria ni faraja kwa Serikali ya sasa kutambua umuhimu wa watoto kwenda shule kwa kutoa elimu ya bila ada, kwani hiyo inasaidia kupunguza watoto wa mitaani.

“Elimu imeleta ukombozi, watoto waliokuwa hawaendi shule walikuwa wanaingia makundini ndipo unasikia Panya Road, mbwa mwitu na mengine,” alisema Mama Maria.

Aidha, alisema ili Taifa lipate maendeleo ni lazima kujiamini, kuthubutu na kutenda kama ambavyo sasa Serikali imejiamini na kuonesha uthubutu katika falsafa ya Hapa Kazi Tu na Tanzania ya Viwanda.

Mama Maria alitoa rai kwa wanawake kushirikiana kuhakikisha wanatunza viwanda vinavyojengwa ili kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa na jamii kwa ujumla.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo