Mwandishi Wetu
Frank Kanyusi |
Maonesho hayo yanatarajia kuanza leo hadi Desemba 11 kwenye
Uwanja wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere, Dar es Salaam.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni (BRELA), Frank Kanyusi, alisema jana Dar es Salaam kwamba maonesho hayo
yanalenga kutekeleza azma ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya
viwanda.
“Maonesho hayo yatatoa fursa kwa viwanda vidogo, vya kati
na vikubwa, kuonesha bidhaa wanazozalisha nchini na pia kutoa hamasa kwa
Watanzania kutumia bidhaa hizo,” alisema Kanyusi.
Alifafanua: “Tunataka wazalishaji kwenye viwanda vya
chini hadi vikubwa, waje waoneshe Watanzania kinachozalishwa, huku tukitarajia
wananchi watahamasika kununua bidhaa hizi zinazozalishwa Tanzania.”
Alisema tukio hilo linalojumuisha wazalishaji,
wafanyabiashara na wananchi ni fursa nzuri ya kutoa huduma zinazohusu uwekezaji
kwenye sekta ya viwanda na biashara, zitakazopatikana kwenye viwanja vya
maonesho na kutolewa na watendaji wa BRELA.
“Hii ni fursa pia kwa washiriki na wananchi kupata huduma
za haraka, za papo kwa papo zinazohusu sekta za viwanda na biashara. Huduma
hizo ni pamoja na usajili wa kampuni, alama na majina ya biashara, utoaji
leseni za viwanda na urasimishaji wa biashara," alisema Kanyusi.
Alisema BRELA itakuwa na banda maalumu litakalotoa huduma
kwenye viwanja hivyo na alitaka washiriki na wananchi wengine wenye kuhitaji
huduma za usajili au leseni za viwanda vidogo na vikubwa, kutumia maonesho hayo
kupata huduma nyingi zitakazotolewa muda wote wa maonesho hayo.
Akizungumzia urasimishaji wa biashara, Kanyusi alisema ni
wakati mwafaka kwa Watanzania kufanya urasimishaji wa biashara zao, kwa lengo
la kuwafanya waendeshe au wamiliki biashara halali na inayotambulika kisheria,
hivyo kuwaondolea usumbufu usiokuwa wa lazima kutoka kwenye taasisi na vyombo
vya Serikali.
Maonesho hayo yameandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa kushirikiana na wadau likiwamo Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNIDO), Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Washiriki wengine wa maandalizi ya maonesho hayo ni Shirika la Maendeleo Tanzania
(NDC), Ukanda Huru wa Uwekezaji (EPZA), Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF),
Kampuni inayojihusisha na alama za biashara ya GSI na wadau wengine kutoka
Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment