*Apongeza mikutano ya hadhara ya kisiasa kuzuiwa
*Asema
ya ndani imekuwa ‘mitamu’, imewaimarisha
Sharifa
Marira
Edward Lowassa |
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward
Lowassa, amesema kwa hali ilivyo na inavyoendelea nchini kuna kila dalili za
chama hicho kushinda uchaguzi mkuu mwaka 2020.
Aidha, Lowassa amesema mikutano ya ndani
ambayo imeruhusiwa na Rais John Magufuli ni ‘mitamu’ zaidi na anashukuru kwa
kiongozi huyo kuzuia mikutano ya nje, kwani ya ndani imesaidia kuwajenga zaidi
kwa kuonana ana kwa ana.
Lowassa alisema hayo jana Dar es Salaam,
wakati kuna kilio kikubwa cha wananchi wanaolia kukabiliwa na hali ngumu ya
kiuchumi, huku wengi wakidhani imesababishwa na kubana matumizi kunakofanywa na
Serikali.
Alisema hayo wakati akifungua semina kwa
wabunge, mameya na madiwani wa chama hicho wa Jiji la Dar es Salaam ikilenga
kujadili kazi waliyofanya ya kutumikia wananchi kwa mwaka mmoja na namna ya
kupiga hatua miaka minne ijayo.
Alifafanua: ”Nimepita maeneo mengi
kufanya mikutano ya ndani, kwa hali ilivyo tunakubalika mno, tuna dalili zote
za kushinda uchaguzi mkuu wa 2020, tujitahidi kuwa na umoja, bila umoja
hatuwezi kushinda ni muhimu sana, CCM wanajua maana ya umoja na
wanaung’ang’ania, tuangalie sana maneno ya kutugawa tusiyakubali.’’
Alisema Chadema itapita maeneo ambayo
watu wako nyuma kielimu ambayo kwa kiasi kikubwa wameipigia kura CCM, ili
kuwaelewesha nia njema ya kuwaletea maendeleo na kuwapa elimu.
‘’Muda uliobaki ni mchache, tunatakiwa
kuamka ili chama chetu kishinde kwa kuwa tumeshakifikisha sehemu nzuri, hatuna
muda tuchangamke kila mmoja aone kwamba anapaswa kueleza namna ya kukisaidia
chama kivuke,’’ alisema Lowassa.
Kuhusu mikutano ya ndani ambayo aliita ‘mitamu’
zaidi, alisema vimefanya wamekuwa imara zaidi, kwani wamezungumza na wanachama
wao maeneo mengi wakiwa wanaonana kwa karibu.
‘’Tumekuwa mikoani na viongozi wenzangu,
tumezunguka mikoani hali ni nzuri kwa mazungumzo tuliyofanya na wanachama wetu,
vikao ni vitamu zaidi kuliko vya nje, unapata nafasi ya kuongea na wananchi ana
kwa ana kwa muda mrefu, kwa mapenzi na mahaba yote,’’ alisema Lowassa.
Lowassa aliwataka mameya na viongozi
wengine wa Chadema jijini humo kukataa kutoa mikataba ya aina yoyote kienyeji
na kushughulikia suala la maegesho, ili isifike mahali wananchi wakajuta
kuichagua Chadema na kusema afadhali CCM.
Zabuni ya maegesho jijini Dar es Salaam
imetolewa kwa kampuni ya Kenya ambayo imeongeza tozo ya kuegesha gari kutoka Sh
300 hadi Sh 500 kwa saa.
Alisema kero ambayo wamekuwa wakikutana
nayo katika mikutano yao ni wananchi kutaka uongozi, jambo ambalo alisema kama
ingepatikana Katiba mpya zingeongezwa nafasi zaidi za kuteuliwa.
0 comments:
Post a Comment