Fidelis Butahe na Charles James
Christopher ole Sendeka |
MWENYEKITI cha CCM, Rais John Magufuli
ameitisha kikao cha Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama
hicho vitakavyofanyika kwa siku tatu Dar es Saalam huku wachambuzi wakibashiri
ajenda kadhaa zitakazoibuka katika vikao hivyo.
Katika kuonesha umuhimu wa vikao hivyo pamoja
na ajenda ya Rais Magufuli kubana matumizi kwa kutosafiri, mkutano NEC ya CCM
utafanyika Dar es Salaam badala ya Dodoma kama ilivyozoeleka.
Ajenda zinazotajwa kuibuka katika vikao
hivyo ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Dimani,
Zanzibar na madiwani katika kata 22 kwenye halmashauri 21 Tanzania Bara,
mabadiliko ya sekretarieti ya chama hicho inayoongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman
Kinana na utendaji kazi wa Serikali iliyoko madarakani.
Nyingine ni madeni ya chama hicho
yaliyotokana na kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana na kuunda Bodi na
Menejimenti ya Uhuru Publications Limited (UPL) inayochapisha magazeti ya
Uhuru, Mzalendo na Burudani.
Taarifa iliyotolewa jana na Seleman
Mwenda kwa niaba ya Msemaji wa Chama hicho, Christopher ole Sendeka, ilieleza
kuwa kikao cha CC kitafanyika kwa siku mbili, Desemba 11 na 12 na kufuatiwa na cha NEC, huku ikihimiza wajumbe wote wa vikao
hivyo kuhudhuria.
Tayari vyama vya siasa vimepewa barua kuhusu
marudio ya uchaguzi wa ubunge Dimani Januari 22 kutokana na kifo cha aliyekuwa
Mbunge wake, Hafidh Ally Tahir huku kampeni zikitarajiwa kuanza Desemba 23 na
kumalizika Januari 21.
Aidha, uamuzi wa Rais Magufuli kuwateua
Dk Emmanuel Nchimbi, Dk Pindi Chana na
Dk Asha-Rose Migiro (wote wajumbe wa Kamati Kuu) na Rajab Ruhwavi ambaye ni
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Bara, kuwa mabalozi, unaashiria chama hicho kuanza
mchakato wa kusaka makada wa kuziba nafasi hizo na pengine kuunda upya Sekretarieti
ya chama hicho.
Akizungumzia vikao hivyo, Dk George
Kahangwa wa UDSM alisema: “Naona utakuwa mjadala wa kujaza nafasi zilizo wazi.
Pia ahadi za Rais Magufuli alizotoa kwenye kampeni pia zitajadiliwa, sambamba
na alizotoa wakati akikabidhiwa uenyekiti wa chama, ikiwamo ile ya kufuta
chipukizi.
“Uchaguzi wa ndani wa chama hicho lazima
utajadiliwa pia, pongezi huenda zikatolewa kwa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo
inaonekana kuwa tofauti na zilizopita, sambamba na kupima utendaji kazi wa
baadhi ya mawaziri,” alisema.
Katika ufafanuzi wake, Dk Kahangwa
alisema chama hicho tawala kinapaswa kujadili hali ya siasa nchini kutokana na
kuminywa kwa demokrasia, akitolea mfano wa kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara,
“Wajitathmini pia kwa kile kilichotokea
Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk Benson Bana alisema: “Suala la uchaguzi mkuu wa CCM linaweza
kujadiliwa katika vikao hivyo, kwa sababu nafasi nyingi ziko wazi.
“Mfano ni ile ya Luhwavi na ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya
Taifa Idara ya Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa iliyokuwa ikishikiliwa na Dk Migiro ambaye kwa sasa ni balozi.”
Alibainisha kuwa baada ya Rais Magufuli
kukabidhiwa kijiti cha uenyekiti na Rais Jakaya Kikwete, aliomba Sekretarieti
iliyokuwapo kuendelea na majukumu yake, hivyo vikao hivyo huenda vikatoa
majukumu kwa baadhi ya wajumbe kupewa dhamana ya uongozi.
“Pia watafanya tathmini ya utendaji kazi
wa Serikali, tutarajie walioonekana kama wasaliti wakiwajibishwa, lakini kwa
njia ya ‘madongo’,” alisema.
Mhadhiri mwingine wa Chuo hicho, Dk
Frank Tily alisema mkutano huu utakuwa na mengi, lakini huenda moja ya ajenda
kuu ikawa ni kupitia mambo yaliyofanywa na Serikali ili kubaini ilipojikwaa.
“Kwa sasa kila mwananchi analia hali
ngumu ya maisha, bila shaka jambo hili litateka zaidi vikao hivyo. Suala la
uchaguzi wa ubunge Dimani lazima itakuwa
ajenda kubwa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment