Dangote hapandishi bei ya saruji—Mwijage


Celina Mathew


SERIKALI imesema saruji haijapanda na kufungwa kwa kiwanda cha mfanyabiashara maarufu wa Nigeria, Alhaji Aliko Dangote, hakuwezi kuathiri bei ya saruji.

Akizungumza na mwandishi wa JAMBO LEO jana kwa simu, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema ni vizuri pia ikaeleweka kuwa kupanda au kushuka kwa bei ya saruji, si ajabu bali ni jambo la kawaida katika biashara, hata wakati kiwanda cha Dangote kilipokuwa kikizalisha.

Waziri Mwijage alifafanua kuwa uwezo wa kuzalisha saruji iliyosindikwa nchini ni tani milioni 10.3, inayozalishwa ni tani milioni 7.1 na mahitaji ni tani milioni 4.3.

“Licha ya kuwapo maeneo ambayo saruji imepanda, lakini kuna maeneo mengine imeshuka, ni suala la kawaida, maana hata jana nilipiga simu Kagera kwa sasa mfuko ni Sh 16,000 na Bukoba Sh 16,000 wakati zamani ilikuwa Sh 22,000,” alisema.

Alisema saruji ipo ya kutosha na nchi ina uwezo wa kuzalisha nyingi zaidi, hivyo kiwanda kimoja kikifungwa hakiwezi kuathiri viwanda 11 vilivyobaki nchini, isipokuwa kitakachotokea ni kwa wanaotumia saruji ya kiwanda hicho ndio wataathirika kwa kiasi kikubwa.

“Suala la kufungwa kwa kiwanda kimoja haliwezi kuathiri vingine ila hapo watakaopata tabu ni wanaonunua na kutumia saruji ya kiwanda hicho hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisema viwanda vyote vinatumia makaa ya mawe ya nchini na uzalishaji wake kwa sasa ni tani 45,000 kwa mwezi.

Alifafanua, kuwa kwa kawaida mawe hayo hayawezi kuzalishwa na kurundikwa, kwa kuwa wakati mwingine husababisha milipuko, hivyo huzalishwa kulingana na maombi ya mtu au kiwanda.

“Makaa ya mawe ya nchini yana ubora na viwango vilivyowekwa kwenye uzalishaji wake, hivyo yapo na yanapatikana kwa wingi, kuna watu wameahidi kuongeza mashine za kuzalishia hivyo hata uzalishaji wake utaongezeka,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo