Chadema: Tutafanya siasa kwa mbinu mbadala


Charles James

Tundu Lissu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema licha ya Rais John Magufuli kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020 kitaendelea kufanya siasa kwa kubuni njia zingine za kukutana na wananchi tofauti na mikutano ya hadhara.

Hayo yamesemwa na Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu, alipozunguza na viongozi 16 wa vyama vya siasa kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao wako nchini kwa ziara ya mafunzo ya kisiasa ambayo yanahusisha pia Chadema.

Lissu alisema ingawa Rais na Polisi wamepiga marufuku maandamano na shughuli za siasa za hadharani bado wao wataendelea kupigana kuhakikisha kuwa haki inapatikana bila kujali kama wanavunja sheria.

“Sisi ni wanasiasa na hiyo ndio kazi yetu, sasa kama Rais amepiga marufuku tufanyeje? Hatuwezi kwenda kanisani eti tukasali ili turuhusiwe kufanya mikutano ya hadhara, tunachofanya ni kubuni mbinu zingine za kukabiliana na watawala na si kujifungia ndani na kukaa kimya,” alisema Lissu.

Alisema njia ambazo Chadema imepanga kufanya kuhakikisha kuwa inaendelea kufikia wanachama na wananchi, ni vikao vya ndani ambapo walianza juma lililopita kwa kanda za Kati na Kusini huku akisema ni endelevu nchi nzima.

Lissu alisema chama chochote cha siasa kinapaswa kujifunza kuishi katika mazingira ya kila aina, hivyo ili kuhakikisha Chadema inaendelea kuwa hai ni lazima ibuni njia mbalimbali za kufanya siasa.

“Vyama vya siasa havipaswi kukaa kimya, inabidi tufuate mfano wa chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC ambacho kilizuiwa kufanya siasa mwaka 1960 lakini kikahimili na hatimaye kutwaa madaraka mwaka 1994, hivyo hata sisi tutahakikisha tunajifungia ndani lakini kimkakati zaidi,” alisema Lissu.

Mkufunzi wa Mafunzo hayo, Christian Echle aliishukuru Chadema kwa kuwapa ushirikiano kwa wiki moja waliokuwa nchini, huku akisema walijifunza vitu vingi kupitia chama hicho.

Mafunzo hayo yalihusisha wanachama na viongozi 16 kutoka Malawi, Angola, Uganda, Afrika Kusini, Senegal, Ghana, Namibia, Msumbiji na watatu kutoka Chadema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo