Watumishi hewa 20,000 waondolewa kwenye mfumo


Sharifa Marira, Dodoma

Jenister Mhagama
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) Angelah Kairuki, amesema Serikali imeondoa kwenye mfumo wake wa ajira, watumishi hewa 19,629 ambao kama wangelipwa mishahara kwa mwezi, wangesababisha hasara ya Sh bilioni 19.749.

Kairuki alisema hayo jana wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Maida Hamad Abdallah (CCM) bungeni jana.

Maida alitaka kujua kiwango cha hasara iliyosababishwa na watumishi hao, ambacho kilibainika kutokana na uhakiki wa watumishi hewa na hatua za Serikali dhidi ya waliosababisha uwepo wa watumishi hao.

“Ningetoa takwimu ya hasara kwa ujumla, lakini ingawa tumeshazipata sijakamilisha kufanya hesabu za majumuisho, hivyo naweza kutoa mifano michache tu kwa kueleza hali ilivyo katika baadhi ya halmashauri na wilaya,” alisema.

Alisema wilaya ya Kinondoni, ilikutwa na watumishi hewa 107 ambao walishalipwa Sh bilioni 1.279 huku Halmashauri ya Kishapu ikikutwa na watumishi hewa 73 ambao walishatafuna jumla ya Sh milioni 543.

Akiuliza swali, Maida alihoji ikiwa pamoja na hatua zinazochukuliwa dhidi ya walioisababishia hasara hiyo, Serikali haioni umuhimu wa watu hao kutakiwa kurejesha fedha zilizopotea?

Akijibu, Kairuki alisema katika mashauri 38 yaliyofikishwa mahakamani na kuhukumiwa, wahusika walitakiwa ama kulipa faini au kurejesha fedha zilizopotea na wanaoshindwa kutekeleza hayo, wanapata adhabu ya kifungo jela.

Alisema majalada 126 yanaendelea kushughulikiwa na serikali inaendelea kuchukua hatua dhidi ya kila anayebainika kuhusika kwa namna yoyote na uwepo wa watumishi hewa serikalini.

Mbunge huyo katika swali lake la msingi, alihoji kauli ya Serikali juu ya  waliohusika kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa njia ya kusababisha uwepo wa watumishi hewa.

Kairuki alisema hadi Oktoba 25 watumishi 1,663 kutoka wizara, idara zinazojitegemea, wakala za Serikali, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa walibainika kusababisha hali hiyo.

Alichanganua kwamba kati ya watumishi hao, 16 ni wa wizara, tisa   idara zinazojitegemea na wakala wa Serikali, sita wa sekretarieti za mikoa na 1,632 wa mamlaka za serikali za mitaa.

“Hadi siku hiyo (Oktoba 25), jumla ya watumishi 638 walikuwa wamefunguliwa mashitaka Polisi, 50 wanafanyiwa uchunguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na 975 wameshitakiwa kwenye mamlaka zao za kinidhamu,” alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo