Mbunge wa Rufiji awatumia salamu mafisadi wa vikoba

Sharifa Marira

Mohamed Mchengerwa
MBUNGE wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM), amesema atashughulika na ufisadi katika vikundi vya kuweka na kukopa vilivyopo katika jimbo hilo ili kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika kwa matumizi sahihi.

Mchengerwa aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa vikoba endelevu ambavyo vimejumuisha vikundi tisa. Hadi sasa vikoba hivyo vina akiba ya zaidi ya Shilingi milioni 45.

‘’Pamoja na jitihada hizi za kuhakikisha tunajikwamua na umasikini kwa kujiunga katika vikundi ili tuweze kusaidiana kirahisi, bado kuna watu ambao wanafanya ufisadi ili kuviua vikundi. Nitakwenda kushughulika nao wote, ikiwa ni njia ya kumuunga mkono rais wetu John Magufuli ambaye kila kukicha anapingana na mafisadi,’’ alisema.

Mchengerwa ambaye baada ya uzinduzi wa vikoba hivyo alichangia shilingi 6,500,000 na kuahidi kutoa milioni mbili zingine, aliwataka wanavikundi hivyo kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika katika maendeleo na kuonya wenye mtindo wa kugawana fedha zinapotolewa.

‘’Naomba fedha hizi zitumike katika matumizi sahihi, nakumbuka hivi karibuni nilitoa pikipiki katika vikundi, lakini taarifa zilizopo ni kwamba watu wameenda kuuza na kugawana fedha jambo ambalo si sahihi. Tunajirudisha nyuma wenyewe,’’ alisema Mchengerwa.

Alisema wananchi wa Rufiji ni maskini na wapo nyuma kimaendeleo, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anakuwa mstari wa mbele kuukataa umasikini huo kwa vitendo.

‘’Nimejitolea kusaidia watu wa Rufiji kwa kuwa mlinichagua ili niwawakilishe. Naombeni kila mmoja aguswe na umaskini tulionao na awe na dhamira ya dhati ya kuutokomeza.”

Aliendelea “Vikundi hivyo vitumike vizuri mkopeshane ili muweze kuendesha na kuanzisha biashara zenu. Naahidi kuwa bega kwa bega na nyie na leo hii (juzi) nawakabidhi mke wangu Farida Mchengerwa kuwa mlezi wenu ili msaidiane naye,’’alisema.

Akizungumza katika tukio hilo Farida aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo kujiunga na vikundi hivyo ili waweze kukopesheka, kwani inajulikana kuwa maskini hakopesheki kutokana na masharti yanayowekwa na taasisi za fedha.

Akizungumza kwa niaba ya wanavikundi wenzake, Abdulrahman Hafidh, alisema vikundi hivyo kwa sasa vina wanachama zaidi ya 220.

Alitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa wanavikundi kuhusu vikoba endelevu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo