Ndege kongwe sasa kutangaza utalii Tanzania


Mary Mtuka

KAMPUNI ya Puma Energy Tanzania inatarajia kutumia ndege 22 za zamani ambazo zimetengenezwa kati ya miaka ya 1920 na 1930 kutangaza utalii wa Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, Philippe Corsaletti   Dar es Salaam jana jukumu la kuendeleza utalii ndani ya nchi, linabaki kuwa sehemu muhimu katika masula ya kijamii.

Alisema katika kufanikisha jukumu hilo kampuni hiyo itakuwa mwenyeji wa ndege hizo za Vintage Air Rally ambazo zitatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Novemba 28 zikitoka Uwanja wa Ndege wa Wilson, Nairobi.

Alisema marubani wa ndege hizo watakapofika nchini watatembelea mbuga za wanyama kama sehemu ya safari yao, hivyo Puma inaamini   itasaidia kuweka utalii kwenye mtizamo wa kimataifa zaidi.

Corsaletti alifafanua kuwa ni kwa sababu ndege hizo zipo kwenye shindano la kuzunguka duniani kuna maelfu ya watu wanafuatilia.

"Kampuni ya Puma tumejiandaa kupokea ugeni huu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma zote za kujaza mafuta ili kuhakikisha urukaji ulio salama. Ndege hizo zinatumia mafuta aina ya Avgas ambayo kwa sasa ni kampuni ya Puma pekee iliyonayo nchini.

Aliongeza kuwa nchini, ndege hizo zitajaza mafuta Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Zanzibar, Dodoma na Songwe kabla ya kwenda Zambia ambako zitapokewa na kuhudumiwa na Puma Zambia.

"Tanzania itaweka historia kwa kuwa moja ya nchi chache duniani ambako mashindano hayo yatapita. Tunawakaribisha wananchi katika tukio hili la kihistoria wakati ndege za Vintage zitakapokuwa zikipita maeneo yenu na kutumia fursa hii kuendeleza utalii," alisema Philippe.

Aliongeza kuwa njia itakayotumika ni sawa na ufuatishaji wa safari ya Shirika la Ndege la Imperial ya mwaka 1931 "Safari ya Afrika" ambapo ndege itakuwa ikiruka chini kupitia Nile kutokea Kongo hadi Khartoum, kupitia nyanda za juu za Ethiopia na uwanda wa chini wa Kenya. 

"Baada ya hapo itaondoka tena kupitia Kilimanjaro hadi Serengeti, na hatimaye kwenye visiwa vya Zanzibar na hadi chini zaidi, kupitia Zambia, juu ya maporomoko ya Victoria, hadi Bulawayo, Zimbabwe," alisema.

"Shindano hili lilianza Novemba 12 Crete, Ugiriki na safari yote itachukua siku 35 kupitia nchi 10 za Ugiriki, Misri, Sudan, Ethiopia, Kenya, Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Botswana na Afrika Kusini. Shindano linalenga kutathmini ujuzi wa marubani husika," alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo