Dangote kutumia umeme wa gesi kuzalisha


Immaculate Ruzika

SIKU moja baada ya kuripotiwa kuwa kiwanda cha saruji cha Dangote kimefungwa, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limesema linafanya jitihada za kuhakikisha kiwanda hicho kinatumia umeme wa gesi kwa uzalishaji.

Taarifa za kufungwa kwa kiwanda hicho zilitolewa jana kwenye vyombo vya habari, zikieleza kuwa kimefungwa kutokana na gharama kubwa ya utumiaji jenereta kuzalisha saruji.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa TPDC,   Kapuulya Musomba alisema walizungumza na Dangote na kukubaliana kutumia umeme wa gesi unaozalishwa Mtwara.

“Mimi nashangaa kuna taarifa zinazushwa, kuwa sisi TPDC ndio tumesababisha Dangote kufunga kiwanda, nasema si kweli sasa hivi tuko kwenye jitihada za kuhakikisha kiwanda kinatumia umeme wa gesi ya Mtwara,’’ alisema.

Musomba alisema Dangote imekuwa ikifanya mazungumzo na TPDC kwa muda mrefu kuhusu bei ya gesi asilia, ambapo iliomba ipewe bei ndogo, ambayo ndiyo inayolipiwa kununulia gesi ghafi kutoka kisimani.

Aidha, Musomba alisema TPDC haiwezi kuuza gesi asilia kwa bei ya kisimani, kwani kuna gharama zinazoongezeka katika kuisafisha na kuisafirisha.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alitabanaisha kuwa TPDC imefanya majadiliano ya mkataba wa awali na kiwanda hicho kwa ajili ya kukiuzia gesi asilia itakayotumika kuzalisha umeme utakaotumiwa na kiwanda.

Musomba aliongeza kuwa inatarajiwa hadi Januari miundombinu ya gesi itakuwa imeunganishwa na mitambo ya kufua umeme, utakaotumiwa na kiwanda.

Kiwanda hicho kinamilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa Nigeria, Aliko Dangote.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo