DC ataka tozo Daraja la Kigamboni ifutwe


Salha Mohamed
 
Daraja la Kigamboni

MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, ameiomba Serikali kuangalia upya tozo za magari ya watumishi wa umma katika Daraja la Nyerere lililoko Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Alitoa ombi hilo jana wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda kuangalia na kutatua changamoto za mkoa huo katika wilaya zake mbalimbali.

Mgandilwa alisema kitendo cha magari ya halmshauri hiyo na watumishi wa umma wanaoishi nje ya halmshauri kutozwa fedha kwa ajili ya kuvuka katika daraja hilo, kinaleta changamoto kubwa na kukwamisha ufanisi.

Alimwomba Makonda kuingilia kati suala la gharama hizo na kuitaka NSSF kuangalia upya tozo kwa magari yote ya halmshauri na magari binafsi ya watumishi wake.

“Kila gari la halmashari linalopita katika daraja hili linatozwa fedha. Hasa ikizingatiwa kuwa halmashauri hii ni mpya, hivyo watumishi wengi wanatokea nje ya halmashauri, hiyo kwa kweli ni changamoto kubwa kwetu,”alisema Mgandilwa.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyrara alikiri kupokea malalamiko ya watu wengi ambao wanataka tozo hiyo iangaliwe upya au kuondolewa kabisa.

“Ni kweli tumekuwa tukipokea malalamiko hayo kutoka kwa wananchi mbalimbali, lakini suala ni kwamba sisi NSSF hatupangi viwango vya tozo za kuvuka daraja bali tunapokea maelekezo kutoka wizara husika (Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi),” alisema Profesa Kahyaraa.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alisema atawasilisha suala hilo katika wizara husika ili kuona uwezekano wa kuondoa tozo hiyo ama kupunguza.

Profesa Kahyarara, alitaja changamoto zingine alizoziona tangu kufunguliwa kwa daraja hilo kuwa ni vijana kuligeuza kuwa kijiwe na wengine kuwa na nia ovu ya kulihujumu kwa kuharibu miundombinu, ingawa ulinzi umeendelea kuimarishwa.

Akizungumzia suala hilo, Makonda alisema suala la tozo ya magari ya halmashauri nam watumishi kuvuka katika daraja hilo atazungumza na waziri mwenye dhamana.

Akihutubia wananchi wanaoishi jirani na daraja hilo, Makonda alisema tayari mkandarasi wa ujenzi wa kipande cha barabara cha kilometa 1.5 inayounganisha daraja la Nyerere atanza kujenga kipande hicho kwa kiwango cha lami.

“Mkandarasi aliyejenga daraja hili ndiyo ataendelea na ujenzi wa kipande hiki kilichobakia.Pesa zipo na ndani ya wiki mbili kuanzia sasa ujenzi utaanza,”alisema.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya alitaja changamoto nyingine zinazoikabili wilaya hiyo kuwa ni kipande cha Kilometa 1.5 cha barabara ya vumbi kutoka katika daraja hilo kuelekea upande wa Kigamboni.

“Hii barabara licha ya kutumiwa na magari mengi, haijajengwa kwa kiwango cha lami, jambo hilo linawapa kero kubwa wananchi kutokana na kusafiri umbali mrefu katika barabara ya vumbi,” alisema Mgandilwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo