Nec: Wanafunzi wawe mabalozi


Hussein Makame, NEC

Mary Longway
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewataka walimu na wanafunzi nchini kuwa mabalozi wa kufikisha elimu ya mpigakura kwa jamii inayowazunguka.

Wito huo umetolewa na Kamishna wa NEC, Jaji mstaafu Mary Longway wakati tume hiyo ilipokuwa ikitoa Elimu ya Mpigakura katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea mkoani Ruvuma, ikilenga kuwawezesha wananchi na wadau wa uchaguzi kufahamu taratibu na hatua zote za uchaguzi hadi kutangazwa kwa matokeo.

“Binafsi nategemea kila mmoja wenu ataweza kumuelimisha mwenzake ambaye hakupata nafasi kama hii ya kujua ni nini elimu ya mpiga kura,” alisema Jaji Longway.

Alisema Elimu ya Mpigakura ikitolewa humwezesha mwanafunzi kupigakura na mgombea mtarajiwa kufahamu sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura au mgombea.

Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa NEC, Emmanuel Kawishe alisema Kifungu cha 61 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinamruhusu mtu kupiga kura kwenye kituo alichojiandikisha na kwamba utaratibu huo huepuka baadhi ya sehemu kuwa na wapiga kura wengi kuzidi uwezo wakati vituo vingine vikikosa kabisa wapiga kura.

Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, Kawishe alizungumzia elimu ya mpiga kura kwa baadhi ya jamii zinazoishi maisha ya kuhamahama sehemu tofauti.

Alisema Tume inawajali wananchi wanaoishi kwa kuhamahama na inawafikia wananchi hao kupitia ushirikishwaji wa asasi za kiraia zinazokwenda kutoa elimu katika maeneo ya jamii hizo ili kuwafikia wananchi ambao ni ngumu kuwafikia.

“Wakati mwingine ili kuyafikia makundi hayo ya wananchi Tume inatumia ngoma na vikundi vya kiutamaduni kwenye maeneo husika, tunatumia redio za jamii za maeneo yale, kwa hiyo asipopata elimu kwa njia hii ataipata kupitia redio na njia za kitamaduni” alisema Bw. Kawishe.

Baadhi ya wanafunzi walizungumzia Elimu hiyo walisema wameridhishwa na Elimu waliyoipata na imewasaidia kufahamu mambo mengi yanayohusu Uchaguzi.

“Kwa kweli sisi wanafunzi wa Songea Girls tumefurahishwa sana kwa kupata elimu ya mpiga kura kwa kuwa imetusaiodia kujua haki zetu kama Watanzania hasa katika masuala ya uchaguzi” alisema mwanafunzi Faraja Samwel Sanga.

Kwa upande wake Husna Banda alisema amefurahi kupata elimu kuhusu kupiga kura na pia amejua umuhimu wa kupiga kura kumchagua kiongozi ambaye anampenda kwa ajili ya maedeleo ya taifa lake.

Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Shule hiyo Tupoke Ngwala alisema wanashukuru kwa nafasi ambayo wameipata ya kupata elimu ya mpiga kura na kwamba anaamini itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi na kuahidi kuifanyia kazi kwa kadri ya uwezo wao ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo