Mtoto aongezeka kilo mbili kila mwezi



Abraham Ntambara

MAMA mzazi wa Antonia Msoka (17) anayeongezeka uzito wa kilo mbili kila mwezi amewaomba msaada Watanzania wamsaidie ili mwanawe atibiwe na kurudi katika hali yake ya kawaida.

Solome Kisusi mkazi wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, akizungumza jana kwnye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) walikolazwa, alisema tatizo la mwanawe lilianza akiwa mdogo.

Alisema alizaliwa alowa na uzito wa kilo 2.3 na baada ya mwezi aliongezeka kilo moja.

"Alizaliwa akiwa na kilo 2.3, baada ya mwezi akaongezeka kilo moja, lakini baada ya hapo kila mwezi akawa anaongezeka kilo mbili," alisema Salome.

Aidha, alisema baada ya kufikisha miezi saba alikuwa tayari na kilo 18, kutokana na hali hiyo kutokuwa ya kawaida walimpeleka hospitali ya wilaya ya Geita ambako waliambiwa hawana uwezo wa kubaini tatizo na kuambiwa waende Bugando, Mwanza.

Salome alifafanua kuwa baada ya kufika Bugando, walifanyiwa  vipimo na vyote vikaonesha hana tatizo hivyo kushauriwa waende  Muhimbili ambako walifanyiwa vipimo na bado hakuonekana na tatizo.

Hivyo, alisema kutokana na hali hiyo waliambiwa warudi waangalie akifikisha miaka mitatu bila kutembea wamrudishe, lakini alitembea hivyo kutokana na hali ya kiuchumi hawakurudi na hawakuwa na hofu sana kwa kuwa mtoto alikuwa anatembea.

Aliongeza kuwa baada ya Antonia kufikisha miaka 12 hali ilibadilika  akashindwa kutembea, akawa anatembea kwa magoti huku akilalamika kuumwa tumbo na miguu kuwaka moto.

Alieleza, kwamba hali hiyo ilipotokea, mwaka jana wakarudi Bugando kufanyiwa vipimo viwili kati ya vitatu alivyoainishiwa ambavyo mmeng'enyo wa chakula na sukari, vyote havikuwa na shida na kilichobaki kilikuwa cha homoni.

Alisema waliambiwa warudi Muhimbili kwa vipimo zaidi ambapo alibainisha kuwa inaonekana kuwa vipimo na matibabu zaidi yatafanyika nje, hivyo akaomba msaada kwa wananchi wamchangie ili kufanikisha matibabu ya mwanawe.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Kisukari na Magonjwa ya Homoni wa MNH, Dk Wolfgang Benard alisema Antonia kwa takribani wiki tatu yuko Muhimbili kwa tatizo lake la kuongezeka uzito kwa kiasi kisicho cha kawaida.

"Uzito huo umekuwa ukiongezeka kila mwezi au kila mwaka na hadi sasa kulingana na uzito alionao kuwa mkubwa, hawezi kutembea kutokana na miguu kushindwa kuhimili uzito wa mwili," alisema Dk. Benard.

Alisema kutokana na kutobaini tatizo, waliamua aletwe Muhimbili ambako walifanya vipimo na vimeendelea kutoonesha kuwa na tatizo lolote.

Alifafanua kuwa tatizo la Antonia halisababishwi na homoni kwa sababu wengi wenye tatizo la namna hiyo chanzo huwa ni homoni ambapo alisema baada ya vipimo hakukuwa na shida ya homoni.

Aidha, alisema wanaona tatizo lake ni jeni ambayo matibabu yake ni upasuaji ambao umekuwa ukifanyika sana nchi za nje na kwamba wagonjwa wanaofanyiwa hivyo hupoteza takribani uzito kwa asilimia 75.

Alisema kwa kuwa Antonia ana uzito wa zaidi ya kilo 150 atakapopasuliwa baada ya miezi mitatu na minne atarudi kwenye kilo kati ya 70 na 80.

Alisema wanaamini baada ya kupungua atatembea tena lakini hakuna uhakika huo kwa kuwa hajatembea kwa muda mrefu, hivyo haiwezi kujulikana miguu itakuwa imeathirika kwa kiasi gani.

Dk Benard alifafanua kuwa kwa sasa wapo katika hatua za mwisho ili kuhakikisha antonio anapelekwa nje kufanyiwa upasuaji.






Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo