Wanaonyanyaswa wakiungana, kete ya upinzani inaimarika



Mashaka Mgeta

Mashaka Mgeta
MOJA ya lugha inayosikika, ikaheshimika na kuzungumzwa na wengi mitaani, ni kwamba ‘kwa utawala wa Rais John Magufuli, heshima imerudi, hakuna wa kujigamba akihoji, unanijua mimi ni nani.’

Umma umejiaminisha kuwa hivi sasa heshima ya utu wa mwanadamu imerejea. Dharau, kiburi ama aina nyingine za unyanyasaji zilizoelekezwa kwa raia, hasa zikiwahusisha ‘vigogo’ wenye mamlaka au dhamana za juu kitaifa dhidi ya wale wa ngazi za msingi vimepungua.

Zile nyakati za Mkurugenzi wa shirika ama taasisi ya umma kutaka aonekane na kuheshimiwa kuliko hata ilivyo kwa Rais wa nchi, zinapita, zinasahaulika na huenda zikafutika na kubaki kuwekwa kwenye vitabu vya kumbukumbu, kwamba vitendo vya aina hiyo viliwahi kutokea.

Mfumo huo unaofanyika sasa chini ya utawala wa Rais Magufuli, unaimarisha Imani ya wananchi kwa Serikali yao, unajenga umoja na mshikamano katikati ya jumuiya za watu, unachagiza kasi ya maendeleo katika mazingira yaliyo rafiki wa amani ya kweli.

Hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli ama wasaidizi hususani Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ‘kuwatumbua’ waliokabidhiwa dhamana ya kulinda rasilimali za umma, badala yake wakazipora na kuzigeuza kuwa zenye kuwanufaisha binafsi, familia na washirika zao inajenga misingi ya usawa.

Kwa hali hiyo, azma na utashi huo vinapaswa ‘kushuka’ kutoka kwa viongozi wan chi hadi kufikia ngazi za msingi kwenye jamii, hususani katika halmashauri za wilaya, miji na majiji.

Ninahusisha maeneo hayo ya utawala wa Serikali Kuu na yale ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa maana mwisho wa siku, kila upande unawajibika kwa raia. Mwananchi anayekatwa
kodi na michango mingine ili kufanikisha uendeshaji wa Serikali, maendeleo na ustawi wa nchi na watu wake.

Hivyo haitakuwa na tija sana ikiwa Serikali Kuu itajiimarisha, itajikita na kuwa na utashi wa kisiasa kuondoa aina za unyanyasaji kwa raia wakati katika ngazi za mikoa na serikali za mitaa, vitendo hivyo vikazidi kushamiri siku hadi siku.

Mamlaka katika ngazi hizo (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) zinapaswa kuhakikisha kuwa utendaji kazi wao hasa katika kuleta haki na usawa kwa raia, unaakisi nia na utashi wa utawala wa awamu ya tano unaolenga kuondoa aina zote za unyanyasaji dhidi kwa wananchi.

Kwa bahati mbaya, ngazi za msingi katika jamii ndipo kunaporipotiwa kutokea `utitiri’ wa unyanyasaji na ukiukwaji wa sheria, unaofanywa na baadhi ya watu wakiwamo viongozi wa Serikali.

Ni katika ngazi hizo kunapotokea vitendo kama vya kuwafungia watu kwenye maghala yanayotumika kuhifadhi mazao ya chakula nay ale ya biashara, wale wanaotuhumiwa kwa makosa yanayopaswa kuthibitishwa na mahakama na si Afisa Mtendaji wa kijiji, mtaa ama kata.

Mathalani kwenye maeneo ya vijijini kulikoaminiwa kuwa na raia walio watii na wenye mapenzi mema kwa Serikali, matukio ya unyanyasaji yanayotokea na kuripotiwa yamekuwa sehemu ya ongezeko la wananchi kusahau mema yanayofanywa na Serikali Kuu, wanabaki kujenga chuki wakiielekea Serikali.

Kutokana na ufahamu wa raia wengi katika ngazi hiyo, ni vigumu kuyatofautisha matendo yanayofanywa na viongozi wa Serikali Kuu na wale wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwao kiongozi wa Serikali ni kiongozi wa Serikali, hivyo unyanyasaji wa aina yoyote unaelekezwa huko.

Ukiachana na maeneo ya vijijini, hata mijini wapo watendaji, watumishi na askari mgambo wanaotekeleza sheria kadhaa za mahali husika, lengo likiwa ni kuweka uhakika wa usalama, Amani na utulivu. Shughuli za uzalishaji na zile za kijamii ziendelee pasipo wasiwasi.

Katikati ya utekelezaji wa majukumu hayo, wahusika wanakutana na watu wa kada tofauti wanaoishi na kufanya shuguli za uzalishaji kwa ajili ya kujikimu na familia zao.

Ni maeneo mengi ya mijini ambapo kuna kundi kubwa la vijana wanaojishughulisha na biashara ndogondogo maarufu kama ‘wamachinga’ ama wanawake wanaopika vyakula katika mazingira magumu ya kutengeneza faida, lakini wakakubali kutambuliwa kwa jina la ‘mama ntilie’.

Makundi hayo mawili, yaani vijana na wanawake, kupitia matokeo ya tafiti mbalimbali yamebainika kuwa na watu wengi walio nguvu kazi kwa nchi na familia zao. Ndio wanaotafuta fedha kwa ajili ya chakula, gharama za nyongeza katika kuwapeleka watoto shule, makazi, mavazi japo kutaja kwa uchache.

Hivyo ‘wamachinga’ wanapofukuzwa, wakapigwa virungu, wakaporwa nguo na mali wanazotegema kuziuza ili fedha zinazopatikana zikalipie pango, kununua sukari, vibaba vya mafuta ya kula, gharama za shule, sadaka na zaka ama mahitaji mengine, wanajijengea fikra ya kunyanyaswa na Serikali.

Kadhalika ‘mama ntilie’ wanaposafiri umbali mrefu kutoka kwenye makazi yao wanapoamka alfajiri, wakiwaacha watoto wamelala, ili wafike maeneo ya biashara zao na kuanza ‘kukoka’ moto wa kuni ama mkaa, wakakanda unga wa ngano kwa ajili ya kupika chapati, maandazi, vitumbua ama kitafunwa chochote.

Wanawake ambao miongoni mwao wanapika supu ya utumbo, nyama, maharage ama chochote kinachotumika wakati wa kifungua kinywa, wanapokutana na ‘rungu la askari wa jiji’, mgambo katika ngazi ya halmashauri au Afisa Mtendaji wa Kijiji au Kata, watabaini kunyanyaswa, kuonewa na kuondoa Imani yao kwa Serikali.

Ndivyo ilivyo kwa hulka  ya mwanadamu anapokuwa katika mazingira yenye ‘kuta za mafarakano’ zinazojenga matabaka ya watu.

0754691540
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo