Ofisi zatakiwa kutumia teknolojia


Mary Mtuka

Dk. Hamisi Kigwangala
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) na ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali zimetakiwa kuhakikisha zinatumia teknolojia za kisasa za ukusanyaji takwimu badala ya kutumia karatasi.

Mwito huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwenye maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika ambayo hufanyika kila Novemba 18.

Alisema matumizi ya teknolojia yataipunguzia Serikali gharama na mzigo wa kudurufu madodoso na kusafirisha mikoani na kuchapishwa makala.

"Kutumika kwa teknolojia kutaendelea kuongeza ubora wa takwimu zote zinazohitajika kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi kwa kuwa hupunguza makosa ya kibinadamu kwa kiasi kikubwa," alisema Dk Kigwangala.

Alisema umuhimu wa kuboresha na kuimarisha takwimu za uchumi na zenye ubora kwa utangamano wa kikanda Afrika utasaidia kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kufanikisha malengo 17 ya maendeleo pamoja na shabaha zake 169 na viashiria 230.

Hata hivyo, alisema ni vema wakahakikisha kuwa wadau kwenye mfumo wa utaoji na utumiaji takwimu wanaungana nao ili kupunguza mitiririko isiyo sahihi ya takwimu.

Mkurugenzi Mkuu wa Takwimu, Dk Albina Chuwa alisema nchi yoyote duniani yenye maendeleo au mabadiliko ya kiuchumi hupimwa kwa takwimu rasmi, kwani wataalamu wa uchumi wanasema ukiboresha takwimu za uchumi umeboresha uchumi wa nchi.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu kwenye maadhimisho hayo iliyotolewa na   Jumuia ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Takwimu Afrika ambayo ni ‘Kuimarisha Takwimu za Kiuchumi kwa Mtangamano wa Kikanda, Mabadiliko ya Miundo na Maendeleo Endelevu', ililenga ukusanyaji na usambazaji wa takwimu za uchumi. 
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo