Benki tatu kiini Bodi TRA ‘kutumbuliwa’


Omary Said, Kibaha

RAIS John Magufuli ametaja kiini cha kuitumbua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akisema ni watendaji kukosa uaminifu kwa kuweka Sh bilioni 26 za Serikali kwenye benki tatu tofauti za binafsi.

Akizungumza katika mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria (OUT), kwenye kijiji cha Bungo kata ya Mkuza Kibaha Mjini jana, Rais Magufuli alisema fedha hizo ziliwekwa kwenye benki hizo kwa lengo la kuzikopeshwa tena kwa Serikali ili zilipiwe riba.

"Baada ya kubaini fedha hizo, tumezirudisha na Bodi husika nimeivunja. Hiyo ndiyo changamoto ambayo Serikali yenu tunapambana nayo. Imani yangu ni kwamba wahitimu, kwa kuwa mnatokea katika nafasi mbalimbali za utumishi wa Serikali, mkitoka hapa mkatusaidie kuwatumikia wananchi ili kuwaondolea changamoto zinazowakabili hatimaye wawe na imani na Serikali iliyoko madarakani," alisema Rais.

Alieleza, kwamba kuna baadhi ya benki zimekuwa zikitumika vibaya kwa kukopesha Serikali fedha zake zenyewe, badala ya kukopesha wananchi na kwamba mambo hayo hukwamisha miradi ya maendeleo.

“Nitaendelea kufanya kazi kwa ufanisi bila kujali itikadi za rangi, dini wala elimu. Nawatumikia wananchi wa hali ya chini, lakini naendelea kuwaomba Watanzania muiunge mkono Serikali katika kuhakikisha wananchi wa hali ya chini wananufaika na rasilimali zilizopo,” alisema Rais Magufuli.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alitangaza kumwondoa Mwenyekiti wa Bodi ya TRA na kuivunja Bodi hiyo katika hatua ambayo haikueleza sababu.

Kuhusu elimu, Rais Magufuli alisema Serikali itaendelea kuboresha sekta ya hiyo, ili iwe ya kiwango cha juu na kwamba katika hilo, hakutakuwa na mjadala, kwani lengo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anayehitimu anakuwa na sifa stahiki.

Alisema katika kuhakikisha hilo alipoingia madarakani, alianza na mchakato wa utoaji elimu bure kuanzia ya msingi mpaka vyuo, jambo ambalo pamoja na juhudi hizo, limekumbana na changamoto za hapa na pale zilizosababishwa na baadhi ya watumishi wasio waadilifu, ambao walikuwa wanaongeza idadi ya wanafunzi hewa.

"Kazi ya kutoa elimu bure ina changamoto zake, ndiyo maana wakati Waziri mwenye dhamana, Profesa Joyce Ndalichako ulipokuwa unazungumzia suala hilo, nami nilikuwa na yangu ya kuzungumza:

“Tangu nilipoingia madarakani na kuanza kutangaza elimu bure kukawa na ongezeko kubwa la wanafunzi hewa, kazi hiyo ililazimika kuwepo upungufu mkubwa wa madawati kazi ambayo kwa asilimia kubwa imefanikiwa, ingawa kuna mikoa michache inaendelea kukamilisha," alisema Dk Magufuli.

Awali, akitoa taarifa ya Chuo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Tanzania, Profesa Samwel Wangwe aliainisha changamoto kadhaa zinazowakabili katika utekelezaji wake wa majukumu yakiwamo ya watu kutotambua maana ya chuo hicho, ambacho malengo yake ni utoaji elimu bila kujali elimu ya mwanafunzi anayehitaji kupata elimu kwenye chuo hicho.

"Chuo hiki kinatoa elimu na leo haya ni mahafali ya 10 ya Chuo hapa makao makuu ya Bungo, madhumuni ni kuwajulisha watu hapa kwamba hapa ndipo kitovu cha Chuo, Kibaha tunatoa elimu ya mifano ya ufugaji kuku wa kienyeji, kilimo na ujenzi,” alisema.

Aidha, Mwenyekiti huyo alimweleza Rais Magufuli kuwa wamepokea vifaa vya Sayansi kutoka Marekani vyenye thamani ya Sh milioni 250 ambavyo vinatumika kwa ajili ya uboreshaji elimu chuoni hapo, ambapo pia chuo hicho kinashiriki Maonesho ya 77 na 88 ya TCU hivyo kuna mwamko mkubwa.

Alisema chuo kilipoanza kilidahili wanafunzi 796, hivi sasa wana uwezo wa kudahili wanachuo wengi zaidi na sasa wamefikia 103,000.

"Kuna changamoto kubwa ya hii barabara, tunaiomba Serikali iijenge kwa kiwango cha lami, kwani inaelekea Soga Stesheni, ikijengwa kwa lami itasaidia kwa kiwango kikubwa katika uboreshaji huduma chuoni na wananchi kwa ujumla, ikizingatiwa soga kuna stesheni ya reli," alisema Mwenyekiti huyo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Elifas Bisanda alisema chuo kinaunga mkono kwa dhati juhudi za Serikali huku wakimwomba asikatishwe tamaa na baadhi ya maneno ya watu wachache.

Naye Waziri Profesa Ndalichako alimhakikishia Rais kuwa wizara yake itaendelea kusimama kidete kuhakikisha vyuo vyote vinatoa elimu bora kwa wanafunzi wenye sifa stahiki na si vinginevyo.

"Tutahakikisha kuna ubora wa vyuo, waendesha vyuo hivyo na wanafunzi wenye sifa stahiki katika elimu husika na hii hata kwa chuo ambacho kinatoa mwanafunzi anayedahiliwa pia ni sifa kwa chuo husika hivyo suala hilo nitalitilia mkazo," alisema Waziri Ndalichako.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo