TBS yawafunda wafanyabiashara


Claudia Kayombo

Dk. Egid Mubofu
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk. Egid Mubofu, ametoa wito kwa jumuia za wafanyabiasha wenye viwanda kuzingatia viwango ili kujipatia uhakika wa soko la ndani na nje ya nchi wanapozalisha bidhaa zao.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Uandaaji wa Viwango wa shirika hilo, Edna Ndumbaro wakati wa maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani, iliyofanyika kitaifa makao makuu ya shirika hilo Dar es Salaam, Dk. Mubofu alisema ni vema wajasiriamali wadogo na wa kati wakaitumia TBS kukuza ubora wa bidhaa.

“Mojawapo ya sababu zinazozifanya bidhaa za nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kushindwa kupenya na kuingia katika masoko ya kimataifa ni kushindwa kukidhi matakwa ya viwango.

“Lakini pia wakati mwingine bidhaa hizo hushindwa kuingia katika soko la kimataifa au la kikanda kutokana na tofauti katika matakwa ya kiwango cha bidhaa husika baina ya nchi na nchi,” alisema Dk. Mubofu.

Aliongeza kuwa shirika hilo linapozidi kusonga mbele, linashirikana na taasisi za kimataifa za viwango kusaidia katika maendeleo ya teknolojia mpya ambazo zitachochea maendeleo ya uchumi na hivyo kuchangia katika ustawi wa Watanzania wote.

Dk. Mubofu alitanabaisha kuwa bidhaa nyingi zinahitaji kufanyiwa vipimo na kutakiwa kukidhi matakwa ya kiwango husika kabla ya kupelekwa sokoni.

Katika biashara zinazohusisha nchi na nchi au mabara, chombo huru kisichoegemea upande wowote kinahitajika ili kukagua mtiririko wa uzalishaji, kufanya vipimo na kuthibitisha ubora wa bidhaa au huduma husika.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo