Bulaya amstaafisha Wasira siasa rasmi



*Yatokana na ahadi yake hivi karibuni
*Yashajiishwa na rufaa kugonga mwamba

Ada Ouko, Musoma

Esther Bulaya
SASA ni dhahiri kuwa Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) amestaafisha rasmi siasa za majukwaani, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Stephen Wasira.

Hatua hiyo imekuja baada ya jana Mbunge huyo kushinda kwa mara nyingine, rufaa aliyokatiwa mahakamani na wanachama wanne wa CCM waliokuwa wapiga kura, wakipinga ushindi wa Esther.

Akisoma hukumu ya rufaa hiyo jana mjini hapa, Jaji Noel Chocha wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, alisema hawezi kufuta matokeo ya uchaguzi huo, uliofanyika mwaka jana, kwa kuwa ushahidi wa waleta maombi haukujitosheleza.

Kesi hiyo ilifunguliwa na wapigakura hao, Magambo Masatu, Matwiga Matwiga, James Ezekiel na Athetic Malagila dhidi ya Esther, ambapo kama rufaa dhidi ya uamuzi wa jana haitakatwa, aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM, Wasira, atakuwa amestaafu rasmi siasa za majukwaani.

Wasira katika mazungumzo maalumu na waandishi wa JAMBO LEO hivi karibuni nyumbani kwake Dar es Salaam, alisema alipanga uchaguzi wa mwaka jana, kuwa wa mwisho kwake kushiriki siasa za majukwaani na baada ya hapo, angestaafu.

Akifafanua hukumu hiyo, Jaji Chocha alisema hakukuwa na tatizo lolote katika vituo ambavyo matokeo yalijazwa kwenye fomu namba 21, wala katika ukusanyaji matokeo ya kila kituo kila kata.

Alisema kama kungekuwa na tatizo, mawakala wa vyama vya siasa wangeandika malalamiko kwenye fomu namba 14, lakini kitu hicho hakutokea.

Jaji Chocha alisema hata madai kuwa Esther hakukidhi vigezo vya masharti ya kujaza fomu ya gharama ya uchaguzi, hayakuthibitishwa mahakamani, kwa kuwa aliyepaswa kufanya hivyo ni Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye kukuletwa mahakamani na hivyo madai hayo hayakujibiwa.

Kwa mujibu wa Jaji Chocha, mbali na kukosekana ushahidi, pia hawezi kufuta uchaguzi huo kwa kuwa wilaya ya Bunda ni masikini na wananchi hawatamudu gharama za uchaguzi unaopaswa kuendeshwa na kodi zao Watanzania.

“Napata taabu kufuta matokeo ya Bunda Mjini kutokana wilaya hiyo kuwa masikini. Wananchi hawatamudu gharama za kuendesha uchaguzi zinazolipwa na Taifa, hivyo kila mlipa kodi ni lazima atoe mchango wake kukamilisha uchaguzi huo,” alisema.

Hata hivyo, Jaji Chocha alisema Msimamizi wa Uchaguzi, Lucy Msofe alifanya uzembe katika kuandika matokeo, baada ya kujaza fomu namba 24 B katika idadi ya wapiga kura waliojiandikisha 164,794 jimboni humo, badala ya 69,369; ambapo hata aliposahihisha alikosea tena na kuandika wapiga kura 69,460 ambayo haikuwa takwimu sahihi.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Wakili wa walalamikaji, Constantine Mtalemwa alidai kuwa wateja wake watakata rufaa, ili haki ikatafutwe maana wameshindwa kuelewa uamuzi uliotolewa na Jaji.

Wakili aliyekuwepo kwa niaba ya Tundu Lisu, akimwakilisha Esther, Paul Kipeja alisema Jaji alitenda haki katika uamuzi wake, hivyo hawana pingamizi lolote.

Kesi hiyo ilifunguliwa Oktoba 18 mwaka jana, katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na kusikilizwa na Jaji Mohamed Gwae, ambaye aliitupilia mbali Januari 25.

Hata hivyo, wapiga kura hao walikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Jaji Gwae, ambayo ilisikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Sirilius Matupa na kutaka maombi hayo yafanyiwe marekebisho maana kulikuwa na tatizo la vifungu vya sheria.

Kesi hiyo ilihamishiwa kwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Rosemary Ebrahim na baadaye kwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jackline Dimelo, kabla ya kusikilizwa Oktoba 3 katika Mahakama Kuu wilayani Musoma mkoani Mara.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo