Mwinyi: Magufuli ni tsunami


*Azungumzia mafanikio yake ya mwaka Ikulu
*Ataka wananchi wamuunge mkono kwa dhati

Fidelis Butahe

Ali Hassan Mwinyi
RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi amempongeza Rais John Magufuli kwa mafanikio aliyopata katika mwaka mmoja madarakani hasa kwa kupambana na rushwa.

Ameifananisha kasi yake ya kupambana na rushwa na dhoruba ya mawimbi ya tsunami yaliyokumba nchi kadhaa duniani miaka 12 iliyopita.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais mstaafu Mwinyi kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Dar es Salaam, tangu kuanza kwa awamu ya tano ya uongozi wake.

"Rushwa ilikuwepo tangu enzi za Nyerere (Mwalimu Julius), aliipondaponda kabisa, lakini hakuimaliza, na sote tuliosalia ni hivyo hivyo, kila mmoja amefanya kwa kiasi chake, lakini Rais Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta tsunami, nafurahi sana," alisema Mwinyi jana baada ya kukutana na Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa iliyotolewa jana ilisema baada ya mazungumzo hayo, Mwinyi alisema lengo la kukutana na Rais Magufuli na kuzungumza naye kwa mara ya kwanza, ni kumpongeza kwa kutimiza mwaka mmoja madarakani na kazi kubwa aliyofanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake.

Alizungumzia Mahakama ya Mafisadi kama moja ya mafanikio yake akisema imekuwa kwenye Ilani ya CCM tangu mwaka 2010, lakini ilizungumzwa zaidi kwenye uchaguzi uliopita na Magufuli akaibeba kwenye kampeni zake, wakati Taifa likipigia kelele ufisadi uliokithiri nchini.

Katika kampeni hizo Rais huyo wa Awamu ya Tano aliahidi kuanzisha Mahakama hiyo kwa lengo la kuhakikisha kesi za aina hiyo zinakuwa na Mahakama yake, kusikilizwa kwa muda mfupi na wahusika kuchukuliwa hatua stahiki.

Baada ya kuapishwa kuwa Rais Novemba 5, Dk Magufuli amepambana na rushwa na ufisadi ikiwa ni pamoja na ‘kutumbua’ baadhi ya watendaji wa Serikali wanaotajwa kwa tuhuma za kutafuna fedha za umma.

Wakati akihutubia Bunge Novemba mwaka jana mara baada ya kuapishwa, Rais Magufuli aliahidi kuanzishwa kwa Mahakama hiyo ambapo Januari alimtaka Jaji Mkuu, Othman Chande kutosubiri Bunge kupitisha Sheria ya Uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi, badala yake waanze maandalizi ya kuiendesha Mahakama hiyo.

Aprili akiwa bungeni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Mahakama ya Rushwa ambayo iliahidiwa na Rais Magufuli wakati wa uchaguzi uliopita, itaanza kufanya kazi hivi karibuni kwa kushughulikia kesi 10 kubwa ambazo uchunguzi wao umekamilika.

Katika mazungumzo hayo, Rais Mwinyi alisema baadhi ya maeneo ambayo Dk Magufuli ameyafanya kwa mafanikio makubwa ni mapambano dhidi ya rushwa na kubainisha kuwa hatua zilizochukuliwa katika kipindi hicho zimedhihirisha kasi kubwa ya kukabiliana na tatizo hilo ikilinganishwa na wakati uliopita.

Alisema eneo lingine ni kuimarisha utendaji kazi serikalini na kwamba hatua zilizochukuliwa na kiongozi huyo wa nchi ziliongeza kasi zaidi huku akitoa mwito kwa viongozi na wananchi kumuunga mkono.

"Tuliobaki tumsaidie, tumsaidie kwa kumwombea dua, tumsaidie kurekebisha kwa kusema ukweli pale ambapo watu wanapotosha, tuseme,” alisema.

“Tusiwaache watu wakapata nafasi ya kusema uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema kutokana na nia yake na lengo lake, lakini hakuna asiyejua kuwa kazi aliyofanya mwenzetu ni nzuri, nzuri, nzuri ya ajabu,” aliongeza.

Katika mwaka wa fedha wa 2016/17 Serikali ilieleza kuwa itaendelea kuchunguza tuhuma 3,444 zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kukamilisha uchunguzi wa tuhuma 10 za rushwa kubwa.

Rais Magufuli pia alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo