Wahitimu wa vyuo wahimizwa kujiajiri


Suleiman Msuya

WAHITIMU wa vyuo nchini wameaswa kujiandaa kukabiliana na changamoto za maisha mitaani kwa kujiajiri na kuachana na dhana ya kuajiriwa.

Hayo yalisemwa jana na mtoa mada katika Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere  (MNMA), Humphrey Sambo wakati akiwasilisha mada iliyobeba jina la Mchango wa Chuo hicho katika ujenzi wa maendeleo ya Taifa.

Sambo alisema ipo dhana ya wahitimu wa vyuo ikiwamo MNMA kujiandaa kuajiriwa na kuacha kutumia taaluma zao kujiajiri.

Alisema elimu waliyopewa wanapaswa kuitumia kikamilifu ili kusaidia jamii ili mchango wa chuo uonekane nchini.

Mtoa mada huyo ambaye pia ni Diwani wa Mbezi na mhitimu wa chuo hicho, alisema amefanikiwa kwa kutumia elimu aliyoipata MNMA.

"Mimi nashangaa sana, mtu anamaliza chuo ana kazi ya kutembea na cheti kutafuta kazi, mbaya zaidi umesoma MNMA, fanya ujasiriamali achana na dhana ya kuajiriwa," alisema.

Alisema mafanikio yoyote katika maisha yanahitaji uthubutu, jambo ambalo linashinda wasomi wengi na kubaki kufanya kazi za kujipendekeza ili wapewe uteuzi.

Aidha, alitaka wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri wa chuo chao waendako na kuachana na tabia ya kulalamika na kuchafua chuo.

Mtoa mada mwingine, Renard Wigira alitaka wahitimu kutambua jukumu lao kwa jamii kuwa ni kusaidia kila sekta.

Katibu wa Baraza hilo, John Muruga alitaka chuo kuongeza miundombinu ili kukabiliana na wingi wa wanaodahiliwa kila mwaka.

Muruga alisema takwimu zinaonesha udahili umeongezeka kwa asilimia 50 hivyo litakuwa jambo la ajabu kubaki na miundombinu ile ile.

"Wakati sisi tunasoma wanafunzi hawakuzidi 3,000 ila sasa nasikia mwaka huu mmedahili 2,363 ni hatua kubwa na tutaendelea kukitangaza chuo," alisema.

Awali akifungua Baraza hilo, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila alisema wanakabiliana na changamoto zilizopo kwa awamu na kutaka wahitimu kuwa mfano sahihi waendako.

Mwakalila alisema wamedhamiria kukirejesha chuo katika lengo lake la awali la kutoa wahitimu viongozi ambao watachangia maendeleo ya nchi. 

"Tumedhamiria kuwa chuo bora chenye kutoa viongozi wasio mafisadi, wala rushwa na wasiopenda kufuata maadili kwani hilo ndilo lengo," alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo