NCCR yapania kufanya maandamano, mikutano


Emeresiana Athanas

Juju Danda
CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema kitafanya mikutano ya hadhara na maandamano ya kichama bila kujali vitisho na porojo zinazotolewa na watawala na Jeshi la Polisi, kwani suala hilo lipo kisheria.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Juju Danda, wakati akitangaza rasmi kuanzisha mpango wa kuimarisha chama kwa mikutano ya ndani, hadhara na shughuli zingine za kisiasa na maandamano nchi nzima yanapohitajika.

Alisema mpango huo unatarajia kuanza wakati wowote baada ya kufuata taratibu na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu mikutano hiyo.

"Mahitaji ya kufanya mikutano hiyo, iko palepale na wakati wowote kuanzia sasa tutatoa taarifa kwa umma," alisema.

Kuhusu suala la kuzuia mikutano ya vyama vya siasa, alisema kauli hizo hazina nguvu, kwani sheria ya kuruhusu kufanyika mikutano hiyo ipo na haijafutwa na hivyo kauli hizo hazina nguvu kisheria.

"Naomba nitoe onyo kwa watawala na vyombo vya Dola kuheshimu sharia, kwani hawako juu ya sheria. Pia polisi lazima watoe ushahidi wa kutosha na taarifa za kuaminika kuzuia mikutano, kwani sababu za kiintelijensia hazina mashiko," alisema.

Aidha, chama hicho hakitavumilia viongozi ambao wamechaguliwa kikatiba na kuapa kulinda Katiba na badala yake kuivunja na kuendesha utawala wa kiimla.

"Kazi inayofanyika kukataza kuendesha vyama vya siasa inatafsirika kuwa ni unyongaji wa vyama vya upinzani," alisema.

Alisema ni vema mamlaka husika ilirejea misimamo na matamko yao ya kukataza mikutano hiyo kupitia sheria ya Jeshi la Polisi na sheria ya nchi, ili waone haja ya kuviachia vyama vya kisiasa kuendelea kufanya mikutano hiyo kikatiba.

Alisema ni vema wanasiasa na vyombo vya Dola kuacha mihemko ya kisiasa na ushabiki ili kudumisha amani ya Taifa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo