Hofu yaendelea kutanda Amboni


Suleiman Msuya

MIEZI sita tangu watu wanane wauawe kwa kuchinjwa katika eneo la Kibatini, Mtaa wa Mlemi, Kata ya Kibatini mkoani Tanga, wakazi wa eneo hilo wameanza kurejea kwa kusuasua, huku hofu juu ya usalama wao ikiendelea kutanda.

Mbali na hali hiyo, ujenzi wa nyumba za wajane wa wanaume waliouawa kwenye tukio hilo umekamilika kwa asilimia 97.

Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlemi, Shaban Muumin alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hii kutoka Tanga.

Mwenyekiti huyo alisema wakazi waliokuwa wakiishi Kibatini hawana amani  na eneo hilo, licha ya kuwa na ulinzi hivyo wanaendelea kuwaelimisha ili wanaotaka warejee.

“Tangu tukio la mauaji ya watu wanane la Mei 30 pale Kibatini wakazi wamekuwa wakisuasua kurejea kwenye makazi yao na familia ambazo wanaume waliuawa zimehamia Kiomoni,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa kwa sasa hali ya Kibatini na Amboni zina utulivu, lakini wananchi bado wana hofu inayosababisha washindwe kurejea kwenye makazi yao.

Alisema inawezekana kusuasua kurejea katika makazi yao kunahusiana na ukweli kuwa tangu tukio litokee hawajapata taarifa rasmi ya wahusika ni nani.

Akizungumzia ujenzi wa nyumba za wajane ambazo ni ahadi ya wabunge wa Mkoa wa Tanga, Meya wa Jiji la Tanga, Selebosi Mustapha alisema hadi jana umekamilika kwa asilimia 97 na kilichobaki ni milango tu.

“Kimsingi sikuahidi kujenga nyumba ila kwa nafasi yangu ya umeya nimefuatilia na wakati mwingine wahusika wanakuja kwangu kufuatilia baadhi ya mahitaji na ninawaekeleza nini cha kufanya,” alisema.

Mustapha alisema katika tukio hilo aliahidi kumsomesha chuo cha ufundi mtoto ambaye alishuhudia baba yake akichinjwa na ameanza kuitekeleza.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Tanga, Lucia Mweru ambaye ni mbunge wa viti maalumu na msimamizi wa utekelezaji wa ujenzi huo, alisema kilichobakia ni milango ambayo Mbunge wa Viti Maalumu mkoani hapo, Ummy Mwalimu ameahidi kuitoa siku yoyote.

Mweru aliwataka wahusika kuwa na subira kwani kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa na hakuna kitakachowakwamisha.

“Kwa sasa tunashughulikia milango ikikamilika nadhani itapelekwa kwani Mbunge Mwalimu anaishughulikia,” alisema.

Alisema nyumba hizo tatu zimejengwa kwa miti na matope na kupauliwa kwa bati na kwamba kila moja inagharimu zaidi ya sh. milioni 3.

Tukio hilo la kinyama lilitokea Mei 30 mwaka huu majira ya saa saba usiku ambapo watu wanane walichinjwa kama kuku na watu wanaosadikiwa kuwa ni magaidi wanaojificha katika mapango ya Amboni.

Waliochinjwa ni Issa Hussein (50), Mkola Hussein (40), Hamis Issa (20) wote wa familia moja, Mikidadi Hassan (70), Mahmood (40), Issa Ramadhan (25 na Kassim.

Issa aliacha mke Mwanaisha Amir na watoto saba ambao ni Hussein, Juma, Amir, Fatuma, Rashid na Ashura ambapo mmoja anasoma Sekondari na watatu shule ya msingi.

Mjane Aisha Said alibainisha kuwa ameachwa na watoto sita ambao ni Abuu, Hessein, Salimu, Ali, Ramadhan na Said.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo