Handeni wanapenda kuzalishwa na kinababa


Mariam Cyprian, Handeni

WANAWAKE wa Wilaya ya Handeni mkoani hapa wamesema hujisikia amani na furaha wanapozalishwa na wauguzi wa kiume waendapo kujifungua hospitali, kwani huwabembeleza wakati wote kuliko ilivyo kwa wanawake wenzao.

Kinamama hao walisema hayo kwenye mikutano ya  uhamasishaji wa jamii kuhusu afya na haki ya uzazi na mila hatarishi iliyofanyika wilayani humo ikiendeshwa na Shirika la Amref Health Africa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni  kupitia  mradi wa Kijana Wa Leo.

Katika mikutano hiyo ya uhamasishaji  iliyofanikiwa kuwafikia na kuwavutia maelfu ya wakazi wa wilaya ya hiyo, mada mbalimbali zilifundishwa na kutolewa ufafanuzi na wawezeshaji tofauti zikijumuisha magonjwa ya ngono na Ukimwi, ukeketaji, uzazi wa mpango, umuhimu wa kuhudhuria kliniki na kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, athari za mimba na ndoa za utotoni.

Wananchi walipata nafasi ya kuuliza maswali na kuelezea uzoefu wao kuhusu maswala mbalimbali ya Afya ya uzazi katika maeneo wanaoishi.

Moja ya swali lililojitokeza ni muuguzi gani wa kike au wakiume wakina mama wanapenda awahudumie wakati wa kujifungua na kutoa majibu kwamba wanapenda kuhudumiwa na wanaume.

Akiuliza swali kwa watalaamu wa afya, mkazi wa Kwachaga, Abdallah Mkorogwe alitaka kujua sababu za wake zao kupenda kuhudumiwa na wauguzi wa kiume licha ya kuwapo pia wa kike kwenye hospitali na sehemu nyingine za kutoa huduma za afya.

Mwelimishaji ambaye ni muuguzi wa kitengo cha afya ya mama na mtoto, Hospitali ya Wilaya Handeni Neema Kombo aliwataka wanawake kujibu swali hilo ni muuguzi yupi wanapenda kuhudumiwa naye wanapokwenda kujifungua?

"Mwanaume ndio anafaa  kwa sababu wanajua kubembeleza, wanajali na kutoa maneno ya faraja hadi mtu anapojifungua lakini hawa wenzetu(wanawake) anakufokea na kukutolea lugha chafu hadi unajutia kubeba mimba," walijibu kina mama hao.

Meneja mradi wa afya  na haki ya uzazi na  ujinsia(Kijana Wa Leo) kutoka Amref Wilaya ya Handeni, Dk. Aisha Byanaku alisema ni haki ya mgonjwa pia kuamua anapenda kuhudumiwa na mtaalamu wa kiume au wa kike anapokwenda kupatiwa huduma hivyo kuwataka wanaume kutokuwa na wasi wasi.

Alisisitiza kuwa Amref kwa kushirikiana na halmashauri  ,wataendelea kutoa elimu ya afya na haki ya uzazi kwa wananchi wa wilaya ya handeni na kuwaomba wananchi kuendelee kushirikiana na shirika kwani, Amref inaamini kuwa wananchi wenyewe ndio kiini cha mabadiliko, kwani wao ndio wanayafahamu vizuri matatizo na changamoto za Afya ya uzazi zinazowakabili, Amref ni muwezeshaji tu.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo