Wasomi: Mambo matano pangapangua ya Magufuli


Fidelis Butahe

Rais John Magufuli
HATUA ya Rais John Magufuli kupangua baadhi ya safu za viongozi aliowakuta na aliowateua katika kipindi kifupi tangu aingie madarakani imewaibua wasomi ambao wametaja kuwa imetokana na mambo makubwa matano ambayo wameyataja.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO wasomi hao walisema kiongozi mkuu huyo wa nchi hufanya mabadiliko anapoona wateandaji hao wanakwamisha malengo yake ili kuifikia dira na mipango aliyokusudia kuitekeleza katika kipindi chake cha uongozi.

Kauli za wasomi hao zimekuja wakati jana asubuhi Rais alimtumbua Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bernard Mchomvu na kuivunja bodi hiyo kabla ya siku hiyo hiyo  mchana kumteua Charles Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, nafasi iliyokuwa wazi kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka jana, Rais Magufuli amekuwa akitengua uteuzi wa nafasi mbalimbali na kuteua watendaji wengine, huku ikielezwa kuwa walioondolewa watapangiwa kazi nyingine.

Hata hivyo, wapo waliopangiwa kazi hizo na wengine kuendelea kusota wakisubiri majukumu mapya, jambo ambalo wasomi hao wamelielezea kuwa na maana kubwa kiutendaji.

Waliyataja mambo hayo matano kuwa ni; uwajibikaji, uzoefu, kasi ya utendaji, kuondoa mazoea kazini na kusaka watu sahihi katika nafasi mbalimbali.

“Hebu tazama pale TRA, hawana jipya mwaka hadi mwaka mambo ni yaleyale ina maana bodi haitoi uongozi na haina dira. Hilo siyo jambo jema kama unataka kuleta maboresho. Unakuwa mwenyekiti wa bodi miaka mitatu hakuna jipya unataka  miaka mingine mitatu? Yaani ukae miaka sita bila jipya. Rais anataka viongozi watendaji sio bora watendaji,” alisema Dk Benson Bana, mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM).

“…Rais anapofanya uteuzi kuna vigezo vingi anazingatia, kwanza uwezo wa mtu pamoja na uzoefu. Hawa wastaafu anaowateua kuwa wenyeviti wa bodi ni watu ambao wana uzoefu, wanaweza kusaidia menejimenti kusonga mbele.”

Alisema uteuzi wa Rais utakuwa na shaka iwapo anayeteuliwa ana historia mbaya ya utumishi.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), Profesa Damian Gabagambi alisema: “Kuongoza ni sawa na kuendesha gari. Huwezi kukariri kwamba kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro utaendesha kwa kasi gani na utakataje kona, inategemea hali ya barabara.”

Alisema Rais kazi yake ni kutazama wapi pamelegea ili apaimarishe huku akisisitiza kuwa mtu anayeshindwa kufanya kazi sehemu moja anaweza kufanya vizuri sehemu nyingine.

“Si jambo zuri kuwaacha watu kukaa sehemu moja muda mrefu hata kama wameshindwa…, inasaidia sana kuongeza ufanisi, unajua Rais amefanya kazi na watu wengi na pia ana vyanzo vingi vya kumpa taarifa juu ya watu wote. Anapomhamisha mtu na kumpangia sehemu nyingine anakuwa na taarifa rasmi, ama ampe kazi nyingine au asimpe,” alisema.

Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu Mzumbe alisema: “Ni sahihi kabisa maana ilifikia mahali mpaka bodi zikawa zinakwenda kufanya vikao nje ya nchi. Utumbuaji huu umewazindua wengi na sasa wanaona kuwa hali imebadilika, kwamba utabaki kama ukifanya kazi, ukishindwa utaondolewa.”

Alisema jambo hilo limerejesha nidhamu katika utendaji wa watumishi wa Serikali na kuongeza tija kwa kiasi kikubwa.
Kuhusu uteuzi kutenguliwa na baadaye wahusika kuteuliwa kushika nafasi nyingine alisema: “Lazima ujue sababu za uteuzi husika kutenguliwa…, kama ukifahamu hilo unaweza kusema Rais alikosea.”

Akitolea mfano kauli iliyowahi kutolewa na Julius Nyerere juu ya kutengua uteuzi wa mtendaji wa Serikali na baadaye kumteua kushika wadhifa mwingine alisema Rais huyo wa Awamu ya Kwanza alitolea mfano wa mtu anayefagia chumba chake kwamba hazuiwi kuokota shilingi na kuirejesha mahala pake, ikiwa atagundua kuwa ilikuwa sehemu ya uchafu uliopo katika chumba hicho.

Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Francis Stolla alisema: “Madaraka ya rais kikatiba ni makubwa na hayana ukomo. Anaweza kumweka mtu katika madaraka na anaweza kumwondoa. Anaweza kutengeneza taasisi na kuziunganisha au kuzivunja.”

Alisema Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alipokuwa madarakani aliwahi kuwajibu wanahabari kuwa ana uwezo wa kumwondoa mtu yeyote hata kama hana tuhuma.

“Kikwete (Jakaya-Rais wa Awamu ya Nne) aliwahi kumwondoa Magufuli (alipokuwa waziri wa Ujenzi) na kumpeleka wizara nyingine. Watu walilalamika ila Kikwete aliwaeleza kuwa anatambua  kuwa Magufuli ni mchapakazi ila alimwondoa ili akafanye kazi nzuri kwingine,” alisema.

Alisema kwa Katiba ilivyo sasa inampa madaraka makubwa Rais kuteua na kuondoa mtu, kuunda taasisi na kuifuta na kusisitiza ni juu ya jamii kuona suala hilo na kuliibua katika mchakato wa kuandika Katiba mpya.

Chekeche
Siku nne zilizopita, Rais Magufuli alimteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.

Uteuzi huo ulifanyika ikiwa zimepita siku 24 tangu alipotengua uteuzi wake katika nafasi ya DCI.

Rais Magufuli miezi 10 iliyopita alitengua uteuzi wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue lakini takribani mwezi mmoja uliopita alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Diplomasia.

Uteuzi wa Sefue ulitenguliwa kwa sababu ambazo hazikutajwa huku akiahidi kumpangia kazi nyingine huku nafasi yake ikijazwa na Balozi John Kijazi.

Rais huyo wa Awamu ya Tano pia aliwaondoa  makamishna wa Jeshi la Polisi, Clodwing Mtweve na Paul Chagonja na kuwateua kuwa makatibu tawala wa mikoa ya Katavi na Mwanza.

Ilielezwa na Ikulu kuwa uteuzi wa makamishna hao wa polisi ni sawa na ule wa Majenerali wa Jeshi la Wananci wa Tanzania kuwa Makatibu Wakuu wa Wizara, kwa lengo la kujenga nidhamu katika utumishi wa umma.

Pia Eliakim Maswi aliteuliwa kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kabla ya kuondolewa na na kurejeshwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, kuelezwa kuwa mabadiliko hayo yalifanyika kwa lengo la kumtafuta mtu mwenye utaalamu wa kuendeleza kazi iliyofanywa na Maswi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo