Lusekelo awachokonoa Lowassa, Sumaye


Leonce Zimbandu

Anthony Lusekelo
MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC) Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa Upako amesema mawaziri wakuu wa zamani  Edward Lowassa, na  Fredrick Sumaye pamoja na kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru  hawakukikimbia chama hicho tawala, bali wamemkimbia ‘mtu’

Akitoa mahubiri jana katika kanisa lake lililopo Ubungo Kibangu Dar es Salaam, siku chache baada ya kuhojiwa na Polisi kwa tuhuma za kutoa lugha ya matusi kwa jirani zake eneo la Kawe, Lusekelo amesema, siyo rahisi kwa vigogo hao watatu kukikimbia chama kilichowalea bali wamemkimbia mtu.

“Si rahisi kukimbia chama kilichowafinyanga  na kuwalea katika safari yao yote ya siasa, hawa wamesoma alama za nyakati, wakaamua kukaa pembeni,” alisema huku mamia ya waumini  wake wakimshangilia.

Lusekelo ambaye hakutaja mtu waliyemkimbia wanasiasa hao wakongwe, alisema kwa kuwa viongozi wa dini wamefanikiwa kuunganisha taifa kwa kuhubiri upendo na amani, Watanzania wasikubali kugawanywa kwa misingi ya siasa.

“Unajua siku moja niliuzwa mimi ni chama gani maana sieleweki, nadhani ningekuwa CCM nisingekamatwa na polisi,” alisema.

Lusekelo ametoa kauli hiyo ikiwa umepita zaidi ya mwaka mmoja tangu Lowassa, Sumaye na Kingunge walipohama CCM, huku kila mmoja akitoa sababu zake kujiengua kutoka chama hicho tawala.

Julai 29, alipokuwa akitangaza kujiunga na Chadema baada ya kujitoa CCM, Lowassa alitaja sababu mbalimbali ikiwamo mchakato wa kuteua wagombea urais kugubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji wa Katiba na taratibu za uchaguzi za chama hicho.

“Niliwekewa mizengwe na kuzushiwa majungu na uongo mwingi, zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo dhahiri na chuki iliyokithiri dhidi yangu. Kikatiba, Kamati ya Maadili si chombo rasmi na haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea Urais kupitia CCM,” alisema na kuongeza:

“Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka Katiba ya CCM, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi pasipo kujali demokrasia, katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM.

Alisema: “CCM siyo mama yangu wala baba yangu ni wakati wa kutekeleza majumu kwa wanachi.”

Agosti22, mwaka jana naye Sumaye alipokuwa akitangaza kuhama CCM mbele ya viongozi wa Ukawa na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema:

“Nimeamua kujiunga na Ukawa ili kusaidia nchi iende kwa kasi kubwa katika kuleta maendeleo ya wananchi ambao wamechoka na wanataka mabadiliko ambayo ni ya dhahiri.”

Kwa upande wake, Kingunge aliyehama CCM Oktoba 5, mwaka jana alisema chama hicho kimepoteza dira na mwelekeo.

“Nimeamua kuchukua uamuazi mgumu kwa kusoma alama za nyakati kutokana na anguko la CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo