Jaji Warioba aombwa kutobadilika


Suleiman Msuya

Jaji Joseph Warioba
WAZIRI Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba ameombwa kubaki na msimamo wake wa kuikosoa Serikali inapokosea, licha ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Maombi hayo yalitolewa na watu wa kada mbalimbali walipozungumza na JAMBO LEO wakisisitiza kwamba Warioba akibaki na msimamo wake wa awali atakuwa ameonesha uzalendo.

Mwanaharakati Renatus Mkinga alisema itakuwa ni jambo la aibu iwapo Warioba atabadilika kwa cheo hicho ambacho ni cha kuteuliwa.

Alisema mtu anayejitambua hawezi kubadilika kisa cheo, hivyo iwapo ataonesha dalili hizo atakuwa hatendei haki wananchi.

“Mimi ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ila sijawahi kuonekana ni kitoka kwenye msimamo wangu na pale ambapo Serikali inapatia nasifia, huo ndio msimamo unaotakiwa,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema haamini kuwa Warioba anaweza kubadilishwa msimamo wake kwa vyeo kwani ana uzoefu mkubwa katika uongozi.

Mtatiro alisema ipo dhana ya viongozi wa Afrika kuwapa nafasi wakosoaji ili wasikosoe Serikali zao, hivyo kwa njia nyingine inaweza kuwa ndilo lengo la Rais.

“Ni vigumu unapokuwa mteule wa Rais uanze kukosoa Serikali yake hata mimi hapa yakinikuta hayo na nikikubali nawajibika kufuata yale ambayo Serikali inafanya,” alisema.

Alisema kiujumla anaona Warioba ameingia kwenye mtego hali ambayo itamshinda kuzungumzia Katiba na mambo mengine muhimu kwa kukosoa.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Onesmo Kyauke alisema kwa nafasi kama ya Warioba kuwa mwoga katika yale ambayo unaamini ni kuondoa uzalendo wako.

“Iwapo angeteuliwa kuwa waziri, katibu mkuu, mkuu wa mkoa au wilaya hayo ambayo yanatajwa kubadilisha msimamo yangetokea ila kwa nafasi hiyo sioni uhusiano,” alisema.

Irene Joseph alisema kwa upande fulani inaweza kuwa njia ya kufungwa midomo iwapo alikuwa anaiomba nafasi hiyo itokee.

Alisema Serikali ya sasa imeonesha dalili za kuhangaika na watu ambao wanaikosoa hasa ambao wako kwenye mfumo, hivyo inawezekana ni mipango ambayo imefanywa kumtuliza, kwani alionesha msimamo katika baadhi ya mambo.
 
Meya wa Kinondoni na Diwani wa kata ya Ubungo, Boniface Jacob alisema kimsingi Warioba alianza kuonesha mabadiliko wakati wa uchaguzi kwa kupigia kampeni CCM, hivyo hana jipya katika kuikosoa Serikali.

Alisema Serikali imeshatambua kuwa watu wengi wenye kuisema wanakabiliwa na njaa, hivyo njia mojawapo ya kuwafunga midomo ni kuwapa nafasi na ndicho kinafanyika.

“Si kwamba nasema Warioba ana njaa, lakini angalia wale CCM ambao walionekana kuwa na njaa wamepewa nafasi sitaki kuwataja, naamini na wewe unawajua,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema kwa mtazamo wake, Warioba anastahili nafasi aliyoteuliwa na hana jipya ambalo anaweza kulizungumza likabadilisha msimamo wa Serikali.

Alitolea mfano Katiba iliyopendekezwa, ilishapita katika mikono yake hivyo na sasa ni mamlaka nyingine inahusika kuikamilisha jambo ambalo Warioba hawezi kubadilisha.

Mwalimu alisema iwapo misimamo aliyokuwa anaisimamia ilikuwa ni ya kizalendo haiwezi kubadilika kwa kigezo cha kuteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo