CUF wageuza Mahakama uwanja wa vita


Grace Gurisha

WAFUASI wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chama hicho,  Maalim Seif Sharif Hamad wamegeuka sinema ya bure baada ya kutwangana makonde hadharani katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Ugomvi huo ulioibua mapambano ya ngumi ulitokea jana baada ya wafuasi wa Maalim Seif waliokuwa mahakamani hapo kumzuia Profesa Lipumba kuingia kusikiliza kesi inayomkabili iliyofunguliwa na Baraza la Wadhamini wa Chama hicho.

Profesa Lipumba alifika mahakamani hapo saa mbili asubuhi, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kesi hiyo dhidi yake kufunguliwa ikidai kuwa yeye si mwanachama halali wa CUF.

Baada ya kesi za Jaji Sakiet Kihio kuitwa na mtoa matangazo wa Mahakama kwa kuelekeza kuwa kesi za Jaji huyo zinasikilizwa chemba watu wote waliinuka na kuelekea katika chumba hicho wakiwamo mawakili wa pande zote.

Walipofika kwenye mlango wa chumba cha Mahakama, wafuasi wa Maalim Seif walisimama mlangoni kumzuia Profesa Lipumba kwa madai kuwa wanaotakiwa ni mawakili tu na si watu wengine, ndipo wafuasi wa Mwenyekiti huyo walipoingilia kati na kuwashushia kipigo watu hao.

Hatua hiyo ilishuhudia mabadilishno ya  makonde na kusababisha watu wawili upande wa Maalim Seif  kuumia, na kusababisha Jaji Kihio kutoa amri kuwa waingie mawakili na walalamikiwa ndipo Lipumba naye akaingia.

Kesi iliendelea kusikilizwa, huku askari wakiimarisha ulinzi wa chumba hicho, kwa sababu wakati wafuasi hao wanapigana wao hawakuwapo. Jaji Kihio aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6 zitakaposikilizwa sababu za Bodi hiyo kumtaka ajitoe kusikiliza kesi hiyo.

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Profesa Lipumba alitolewa na wafuasi wake akiwa chini ya ulinzi mkali kwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu atakayemgusa na alipofika nje, alipokewa na wafuasi wengine wakiwa na mabango yenye ujumbe dhidi ya Maalim Seif.

Bango moja liliandikwa: ‘Maalim Seif kama ulikaa na CCM umeshindwaje kukaa na Mwenyekiti wako Lipumba mkayamaliza’, linguine: ‘Maalim Seif tulijua CCM ndiyo kiboko yako, kumbe Lipumba ndiye mwamba wako’, huku wakiendelea kuimba wimbo wa chama hicho.

Lipumba alipoingia kwenye gari alishusha kioo na kusalimu wafuasi wake kwa kuwapungia mikono, huku wengine wakisukuma gari lake kabla ya kuondoka eneo la Mahakama.

Hata hivyo, Profesa Lipumba hakutaka kuzungumza chochote, akitumia muda wake mwingi kutabasamu na kupunga mkono. Wakati hayo yote yakifanyika, nje ya Mahakama askari walikuwa tayari wametenga makundi hayo mawili, lakini bila kufanya hivyo, watu hao wangeendelea kupigana.

Wakili wa Bodi hiyo, Juma Nassoro akiwa nje ya Mahakama, alimkariri Jaji akisema Desemba 6 kesi hiyo ataisikilizia kwenye Mahakama ya Wazi, kwa sababu alikuwa hajui kama watu ni wengi, kwa hiyo hataifanyia tena chemba.

Pia alisema Profesa Lipumba, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na wafuasi 11 wamewasilisha pingamizi mahakamani hapo, kuwa wateja wake walifungua kesi hiyo bila idhini ya Mahakama na pia Maalim Seif alibariki kufunguliwa kwa kesi hiyo bila idhini ya Bodi.

Baadaye mawakili wa CUF, Nassor na Hashimu Mziray waliwasilisha ombi la kumtaka Jaji Kihiyo ajitoe kusikiliza shauri hilo kwenye Mahakama hiyo, na sababu za kumkataa zitaelezwa Desemba 6 saa saba mchana wakati kesi hiyo itakapokuja kusikilizwa.

Walalamikaji hao wanaomba Mahakama itengue barua ya Msajili ya kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwanachama hai wa CUF.  Wakili Mziray alisema walifungua kesi hiyo kwa hati ya dharura kutokana na mambo yalivyo sasa ndani ya chama hicho, kwa sababu hawajui hata ofisi zingine zinaendeshwaje.

Alisema katika maombi hayo, wanaiomba Mahakama mambo matatu, ambayo ndiyo yanasababisha kufukuta kwa mgogoro, kwa hiyo wanaomba yatenguliwe ili shughuli za kisiasa ziendelee.

Alisema mambo hayo ni pamoja na Mahakama kutengua barua ya Msajili ya Septemba 23 ambayo ilitengua uamuzi wa CUF wa kumfukuza uanachama Profesa Lipumba na kumhalalisha kuwa mwanachama hai wa chama kama Mwenyekiti.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo