Ansaf kukutanisha wadau kujadili viwanda


Mwandishi Wetu

MABORESHO ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati itafanikiwa ikiwa Serikali itaboresha sera za sekta hiyo na kuweka mazingira yanayovutia uwekezaji kwa wazawa na wageni.

Tangu aingie madarakani, Novemba 5 mwaka jana, Rais John Magufuli amekuwa akihimiza kubuniwa na kutekelezwa kwa mipango ya kujengwa viwanda ili pamoja na mambo mengine, vichangie kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Katibu Mtendaji wa shirika lisilo la Serikali la Wadau wa Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge amesema azma hiyo inapaswa kutekelezwa kwa kutoa kipaumbele kwa viwanda vidogo visivyohitaji mitaji mikubwa, vikitoa ajira nyingi na kuwa karibu na wananchi wa ngazi za chini kwenye jamii.

Rukonge alisema hayo jana ofisini kwake Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa ya kongamano la wadau wa kilimo litakalofanyika Dodoma Desemba mosi na 2, likijielekeza katika nafasi ya kilimo kwenye viwanda.

“Hatutaipeleka nchi kwenye ushindani wa viwanda ikiwa mkakati wetu hautaiwezesha sekta ya viwanda vidogo kushamiri, ili kuzalisha bidhaa zitakazochatuliwa na viwanda vya kati kabla ya kufikia vikubwa,” alisema.

Pamoja na maboresho ya viwanda, Rukonge alisema uboreshaji wa miundombinu na sera yanapaswa kutoa jawabu la kulinda mazao yanayozalishwa nchini bila kuathiri taratibu za Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO).

Alisema nchi kadhaa duniani zinatekeleza mahitaji ya kisera kulinda bidhaa za ndani zikiwamo za kilimo, kama ilivyo India inavyotoza asilimia tano kwa korosho inayoingizwa kutoka nje ya nchi hiyo.

“Hivi sasa uzalishaji wa korosho India umeongezeka kwa kiasi kikubwa hivyo kuifanya nchi hiyo kutoza asilimia tano ya thamani ya korosho inayoingizwa kutoka nje ikiwa katika hali ghafi, ili kulinda korosho wanayozalisha,” alisema.

Pia Rukonge alisema pamoja na kulinda uzalishaji wa ndani, ipo haja ya kuwapo ruzuku kwa wakulima ili kukuza uzalishaji, akitoa mfano wa Umoja wa Wabanguaji Wadogo wa Korosho nchini, asilimia 70 ya wanachama wake wakiwa ni wanawake.

Azimio la Maputo la Mwaka 2003 lililosainiwa na wakuu wa nchi za Afrika, lilihimiza kutengwa kwa bajeti za mataifa hayo kufikia asilimia 10, ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo ambayo uchumi wake unategemewa na takribani asilimia 80 ikihusu watu wanaoishi vijijini.

Kuhusu kongamano la Dodoma, Rukonge alisema limejielekeza katika masuala ya kilimo kwenye viwanda, kutokana na azma ya Serikali ya awamu ya tano kutilia mkazo mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa yenye uchumi wa viwanda.

Kongamano hilo litajumuisha washiriki wanaokadiriwa kufikia 150 wakiwamo watafiti watakaowasilisha matokeo ya utafiti wao kuhusu sekta za kilimo na kiwanda.




Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo